Kaburi jengine la halaiki lagunduliwa katika mkoa wa al-Anbar, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60203-kaburi_jengine_la_halaiki_lagunduliwa_katika_mkoa_wa_al_anbar_iraq
Vikosi vya usalama vya Iraq vimegundua kaburi la halaiki lenye maiti za askari wa usalama na raia waliouawa katika mkoa wa al-Anbar magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 06, 2020 03:35 UTC
  • Kaburi jengine la halaiki lagunduliwa katika mkoa wa al-Anbar, Iraq

Vikosi vya usalama vya Iraq vimegundua kaburi la halaiki lenye maiti za askari wa usalama na raia waliouawa katika mkoa wa al-Anbar magharibi mwa nchi hiyo.

Idara ya Intelijensia ya Jeshi ya Wizara ya Ulinzi ya Iraq imeeleza katika taarifa kwamba, katika operesheni iliyofanywa na vikosi vya usalama ya kuteketeza maficho 29 ya magaidi wa kundi la ukufurishaji la DAESH (ISIS), limegunduliwa kaburi moja la umati lenye maiti za askari wa vikosi vya usalama pamoja na raia katika kitongoji cha Hait, magharibi wa mkoa wa an-Anbar.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vikosi vya usalama vya Iraq vimeshambulia maficho ya magaidi wa Daesh katika eneo la al-Khaudhah kwenye kitongoji cha Hait na kufanikiwa kugundua na kukamata pia kiwango kikubwa cha zana za kijeshi.

Novemba mwaka 2018, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa kundi la kigaidi la Daesh limeacha makaburi zaidi 200 ya halaiki katika maeneo mbalimbali ya Iraq liliyokuwa limeyavamia na kuyakalia kwa mabavu kati ya mwaka 2014 hadi 2017.

Kwa msaada wa fedha na silaha wa Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na wa Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, mwaka 2014 kundi la kigaidi la Daesh lilishambulia na kuyakalia maeneo mengi ya ardhi ya Iraq na kutenda jinai za kinyama zisizohesabika katika maeneo hayo.

Hata hivyo kwa msaada wa washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mnamo Novemba 17, 2017 vikosi vya Iraq vilifanikiwa kuukomboa mji wa Rawa, ulioko mkoani al-Anbar, ambao ulikuwa ndio ngome ya mwisho ya kundi hilo la ukufurishaji na kusambaratisha kikamilifu uwepo wa kundi hilo nchini humo.../