UN yapongeza usitishaji vita Yemen, yataka uheshimiwe
-
Martin Griffiths
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen pamoja na Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi wamepongeza uamuzi wa kusitisha vita na mapigano nchini Yemen.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Martin Griffiths, Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen alielezea hisia zake hizo jana na kuitaka Saudi Arabia na pande nyingine zinazohusika na mapigano huko Yemen kuacha uadui na kuheshimu uamuzi huo wa kusimamisha vita.
Kwa upande wake, Nayef Falah al Hajraf, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi naye ameelezea matumaini yake ya kuheshimiwa uamuzi huo wa kusimamisha vita na kutekelezwa mwito wa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen wa pande zote kuacha uadui na kufikia makulibano ya kudumu ya kusimamisha vita.
Hata hivyo, muungano vamizi wa Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) tayari umevunja usitishaji vita katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
Juzi Jumatano mchana muungano huo vamizi ulitangaza kile ulichodai ni 'usitishaji vita' katika mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Yemen. Hata hivyo usiku wa hiyo hiyo Jumatano, ulikwenda kinyume na tangazo lake hilo kwa kushambulia kwa mabomu maeneo kadhaa ya nchi hiyo ya Waislamu.
Kabla ya mashambulizi hayo, Harakati ya Ansarullah ilikuwa imesema kuwa haina imani na tangazo hilo kwani muungano huo vamizi hauna tabia ya kuheshimu maneno yake. Aidha ilisema, hiyo ni mbinu tu ya utawala wa kiimla wa Aal Saud ya kujaribu kujipapatua kutoka katika kinamasi cha Yemen bila kufedheheka zaidi.