Seneta wa Marekani akiri kushindwa Saudia katika vita vya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60348-seneta_wa_marekani_akiri_kushindwa_saudia_katika_vita_vya_yemen
Seneta mmoja wa Marekani amekiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kushindwa Wasaudi katika vita vya kichochezi dhidi ya watu wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 13, 2020 06:27 UTC
  • Seneta wa Marekani akiri kushindwa Saudia katika vita vya Yemen

Seneta mmoja wa Marekani amekiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kushindwa Wasaudi katika vita vya kichochezi dhidi ya watu wa Yemen.

Seneta Chris Murphy wa jimbo la Connecticut nchini Marekani aliwakejeli Wasaudi kupitia ujumbe wa mtandao wa kijamii wa Twitter aliouandika siku ya Jumapili kwamba baada ya kuvuruga kwa miaka kadhaa mapatano ya amani ya Yemen, hatimaye Wasaudi wameanza kutafuta njia za kujitoa nchini humo.

Murphy amesema, katika mazingira ya sasa ambapo virusi vya corona vinaenea kwa kasi duniani, ni muhimu kwa pande zinazozozana kutafuta njia za kisiasa kwa ajili ya kutatua tofauti zao na hivyo kuzuia kuenea kwa virusi hivyo ambavyo vimeangamiza watu wengi ulimwenguni.

Baadhi ya droni za Yemen ambazo zimetoa pigo kubwa kwa Saudia katika medani ya vita

Jumatano iliyopita utawala wa Saudia ulichukua hatua ya upande mmoja ya kusitisha vita nchini Yemen kwa muda wa wiki mbili.

Licha ya madai hayo ya kusimamisha vita, lakini muungano wa vita unaoongozwa na utawala huo dhidi ya Yemen umeendelea kuishambulia nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Siku ya Jumapili usiku, msemaji wa jeshi la Yemen alisema kwamba katika kipindi cha masaa 72, ndege za kivita za Saudia zilishambulia zaidi ya mara 100 maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imesema kuwa kutangazwa usitishaji vita huo wa upande mmoja ni dalili ya kushindwa muungano huo wa kivita wa Saudia na kwamba umetangaza usitishaji vita huo wa wiki mbili ili upate muda wa kupumua na kupunguza mashinikizo unaokabiliwa nayo.