Utawala haramu wa Kizayuni na mkosi wa jina 'Netanyahu'
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60470-utawala_haramu_wa_kizayuni_na_mkosi_wa_jina_'netanyahu'
Duru za habari za utawala haramua wa Kizayuni zinasema kwamba Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala huo ametishia kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba iwapo mahakama itamuuzulu kwenye nafasi yake hiyo, basi atachochea uasi wa mitaani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 19, 2020 04:57 UTC
  • Benjamin Netanyahu, Hitler wa sasa
    Benjamin Netanyahu, Hitler wa sasa

Duru za habari za utawala haramua wa Kizayuni zinasema kwamba Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala huo ametishia kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba iwapo mahakama itamuuzulu kwenye nafasi yake hiyo, basi atachochea uasi wa mitaani.

Mwenendo wa kuundwa baraza la mawaziri la utawala huo kwa mara nyingine umekumbwa na mkwamo. Baada ya kufanyika uchaguzi wa bunge wa duru ya tatu katika mwaka mmoja, Benny Gantz, Kiongozi wa Muungano wa Blu na Nyeupe alitakiwa kuunda serikali, hata hivyo katika muda wa kisheria na hata pamoja na kuongezwa masaa 48, hakuweza kuunda serikali hiyo. Katika uwanja huo, Alkhamisi iliyopita Reuven Rivlin, Rais wa utawala wa Kizayuni alituma barua akiwataka wabunge wa Knesset wamteue waziri mkuu wa utawala huo. Katika barua hiyo Rivlin aliwahutubu wabunge kwa kusema: "Ni matumaini kuwa wajumbe wa Knesset wataweza kwa wingi wao kufanikisha uundwaji wa baraza la mawaziri haraka iwezekanavyo, ili kuepusha uchaguzi mwingine wa nne." Tatizo kubwa katika kadhia ya kuundwa serikali mpya ya utawala wa Kizayuni, ni mienendo hasi ya Benjamin Netanyahu. Netanyahu anakabiliwa na tuhuma nyingi za ufisadi. Yapata mwezi mmoja na nusu uliopita ambapo Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Utawala wa Kizayuni aliwasilisha jina la Netanyahu kwa mahakama ya utawala huo unaokalia Quds Tukufu kwa mabavu na hivyo kiongozi huyo kuwa waziri mkuu wa kwanza katika historia ya miaka 72 ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina, kuburuzwa kwenye mahakama kwa tuhuma za kupokea hongo, ulaghai na uhaini.

Benjamin Netanyahu 

Kikao cha kusikiliza kesi ya Netanyahu kilipangwa kufanyika tarehe 17 mwezi Machi 2020, lakini mahakama hiyo ikaakhirisha kikao hicho kwa sababu za kuenea virusi vya Corona. Hivi sasa Netanyahu anafanya njama ya kuendelea kubakia madarakani katika wadhifa wa waziri mkuu au angalau apate dhamana itakayomlinda baada ya kumalizika muda wa uongozi wake, asiweze kutupwa jela. Katika uwanja huo, Netanyahu ameunda mtandao mkubwa wa siri kati ya waungaji mkono wake katika muundo wa utawala wa Kizayuni hususan ndani ya bunge na hata ndani ya chama cha Likud, ambao unafanya juhudi za kuufanya kuwa mgumu mwenendo wa kumuondoa madarakani. Ndani ya bunge la utawala wa Kizayuni, waungaji mkono wa Netanyahu wanazuia kuundwa kwa wingi mutlaki wa asilimia 50+1 (yaani wa viti 61) kwa maslahi ya washindani wake, kwani jambo hilo ndilo litakalomuwezesha kuendelea kubakia madarakani.

Netanyahu ambaye ni tishio kwa utawala wa Kizayuni

Licha ya nafasi ya chama cha Likud ndani ya Israel kukumbwa na hatari, lakini katika uchaguzi wa ndani ya chama uliofanyika mwezi Disemba mwaka jana, kwa mara nyingine Netanyahu aliweza kuibuka mshindi na hivyo kuendelea kukiongoza chama hicho. Hivi sasa wakati ambapo kwa mara nyingine suala la kufanyika kikao cha kusikilizwa kesi inayomkabili waziri mkuu huyo linajadiliwa, Netanyahu ametishia kuchochoea uasi dhidi ya mahakama kuu ya utawala bandia wa Kizayuni. Katika uwanja huo gazeti la Kizayuni la Haaretz limeandika kwamba, Netanyahu ambaye anakabiliwa na mafaili matatu ya ufisadi wa kiserikali na tuhuma rasmi katika mahakama, kupitia mazungumzo ya faragha ametishia kuanzisha uasi wa mitaani dhidi ya mahakama kuu iwapo atauzuliwa katika nafasi yake ya waziri mkuu. Kwa hakika mwenendo wa Netanyahu katika mchakato wa kuundwa serikali na pia katika suala la mafaili ya ufisadi unaonyesha kuwa, waziri mkuu huyo wa utawala haramu wa Kizayuni, ameunda magenge ya siri kwa lengo la kumsaidia kubakia madarakani ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.