Wanamgambo wa Imarati wajitangazia uhuru kusini mwa Yemen; Answarullah yalaani
Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amelaani hatua ya wanamgambo wa Umoja wa Falme za Kiarabu ya kujitangazia uhuru huko kusini mwa Yemen na kusema kuwa, hatua hiyo ni kutangaza kujitoa kikamilifu wanamgambo hao katika makubaliano ya Riyadh kati yao na serikali iliyojiuzulu ya Abdu Rabbuh Mansour Hadi.
Usiku wa kuamkia leo Jumapili, wanamgambo wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wanaojiita Baraza la Mpito la Kusini (STC) wametangaza kuwa, kuanzia sasa watakuwa wanasimamia na kuendesha kivyao masuala ya mji wa bandari wa Aden na mikoa mingine ya kusini mwa nchi hiyo na tayari wametangaza hali ya hatari katika maeneo hayo.
Muhammad Ali al Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen ambaye ni katika viongozi wa ngazi za juu wa harakati ya Answarullah ameiambia serikali iliyojiuzulu ya Abdu Rabbuh Mansour Hadi kwamba, nyinyi muda wote mumekuwa mukidai kuwa eneo la kusini mwa Yemen liko mikononi mwenu, haya sasa tekelezeni makubaliano chapwa ya Riyadh na wazuieni wanamgambo wa Imarati kujitangazia uhuru kusini mwa Yemen.
Mikoa mingine ya nne ya kusini mwa Yemen pia imepinga uamuzi huo wa wanamgambo wa Imarati na kuuita kuwa ni mapinduzi ya kijeshi dhidi ya makubaliano ya Riyadh na ni kinyume na Katiba.
Makubaliano ya Riyadh ni makubaliano yaliyofikiwa baina ya wavamizi wa Yemen, yaani Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Wavamizi hao walifikia makubaliano hayo ili kugawana madaraka katika maeneo ya kusini mwa Yemen. Hata hivyo makubaliano hayo yalivunjwa mwanzoni kabisa mwa kufikiwa kwake na tangu wakati huo harakati ya Answarullah iliyaita kuwa ni makubaliano chapwa yasiyo na chochote cha maana ndani yake.