Sababu za kudhihiri tena Daesh nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60771-sababu_za_kudhihiri_tena_daesh_nchini_iraq
Magaidi wa kundi la Daesh wameshambulia Harakati ya Wananchi wa Iraq Hashdu Sha'bi, na kuua pamoja na kujeruhi makumi ya wanaharakati wa kundi hilo la mapambano ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 04, 2020 09:54 UTC
  • Sababu za kudhihiri tena Daesh nchini Iraq

Magaidi wa kundi la Daesh wameshambulia Harakati ya Wananchi wa Iraq Hashdu Sha'bi, na kuua pamoja na kujeruhi makumi ya wanaharakati wa kundi hilo la mapambano ya Kiislamu.

Katika mapigano makali yaliyojiri alfajiri ya tarehe pili Mei, magaidi wa Daesh walivamia na kushambulia vituo vya harakati ya Hashdu Sha'abi katika maeneo ya Balad na Mikeishifa kusini mwa mji wa Tikrit na kaskazini mwa Samarra katika mkoa wa Swalah Deen, ambapo waliua shahidi wanaharakati 10 na kuwajeruhi wengine wanne wa kundi hilo. Jana Jumapili pia magaidi hao walivamia kituo cha polisi kaskazini mashariki mwa Dayala na kuua pamoja na kujeruhi maafisa 13 katika kituo hicho.

Ni muhimu kutaja hapa nukta kadhaa kuhusiana na tishio la kudhihiri tena kundi la Daesh nchini Iraq.

Nukta ya kwanza ni kuwa kundi hilo la kigaidi limelenga vijiji kadhaa vilivyogurwa katika mikoa ya Dayala na Swalahu Deen kwa ajili ya kuhuisha shughuli zake za kigaidi katika ardhi ya Iraq. Vijiji hivyo kimsingi havina wakaazi na vinapewa uzingatiaji mdogo na askari usalama wa Iraq.

Kwa msingi huo ni rahisi kwa magaidi kupanga na kutekeleza operesheni zao za kigaidi katika maeneo hayo. Katika uwanja huo, kamanda wa Hashd Sha'bi katika maeneo ya wafugaji amesema kuwa vijiji vilivyohamwa vimegeuka na kuwa vituo vya kupanga njama na kuvutia magaidi wapya wa Daesh katika mkoa wa Dayala.

Marekani inashirikiana kwa karibu na Daesh kuvuruga usalama wa Iraq

Nukta ya pili ni kwamba Daesh imeanzisha mashambulizi hayo sambambva na kuongezeka mashinikizo ya kuitaka Marekani iondoe askari wake katika ardhi ya Iraq. Tarehe 5 Januari mwaka huu ikiwa ni siku mbili tu baada ya kuuawa shahidi kamanda wa mapambano ya Kiislamu, Qassem Suleimani, bunge la Iraq lilipitisha mswada wa kufukuzwa nchini humo askari vamizi wa Marekani.

Wananchi na makundi mbalimbali ya Iraq pia katika siku za karibuni yamekuwa yakishinikiza askari hao waondolewe nchini humo haraka iwezekanavyo na kutekelezwa sheria iliyopitishwa na bunge la nchi hiyo kuhusu suala hilo.

Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa na vilevile shakhsia mbalimbali wa Iraq wanasema kuwa harakati za Daesh zimeongezeka nchini humo kutokana na mipango na njama za Marekani ili kuwafikishia wananchi, makundi ya kisiasa na serikali ya Iraq ujumbe huu kwamba iwapo askari wa nchi hiyo ya Magharibi watafukuzwa nchini humo basi nchi hiyo itakumbwa na ongezeko la vitendo kama hivyo vya magaidi wa Daesh. Kwa ibara nyingine ni kuwa Marekani inafanya njama za kuendelea kubakia Iraq kwa kushirikiana na Daesh katika kutekeleza ugaidi dhisi ya watu wa Iraq.

Kuhusu suala hilo Muhammad Mahdi al-Bayati, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa Taasisi ya Badr ya Iraq anasema: Mashambulio ya kigaidsi ya hivi karibuni nchini Iraq yametekelezwa kwa uungaji mkono na ushirikiano kamili wa Saudi Arabia na Marekani kwa sababu nchi mbili hizo zinafanya juhudi za kuwarudisha magaidi wa Daesh katika ardhi ya Iraq.

Muhammad Mahdi al-Bayati

Nsssir as-Shamri, Msemaji wa Harakati ya Nujabaa ya Iraq pia amesisitiza: Kila mara linapojadiliwa suala la kuondolewa wavamizi wa Marekani nchini Iraq, vitendo vya ugaidi navyo huongezeka.

Nukta ya tatu ni kuwa kuongezeka vitendo vya magaidi wa Daesh nchini Iraq kuna uhusiano wa moja kwa moja na hali tata ya kisiasa iliyoko nchini humo. Tangu mwezi Disemba mwaka uliopita hadi sasa Iraq imekuwa ikiendeshwa na serikali ya muda, na Mustafa Al-Kadhimi bado hajafanikiwa kuunda serikali. Pengo hilo la kisiasa ni fursa nzuri kwa kundi hilo la kigaidi kujiimarisha huko Iraq. Serikali ya hivi sasa ya Adel Abdul Mahdi imeshughulishwa na mapambano dhidi ya janga na virusi hatari vya corona na hivyo kuwa na muda mdogo wa kuzingatia hatari ya Daesh.

Katika uwanja huo, Hassan Karim al-Ka'bi, Naibu wa Kwanza wa Spika wa Bunge la Iraq anasema: Kundi la kigaidi la Daesh linatumia vibaya hali ya hivi sasa ya kisiasa na mapambano dhidi ya virusi vya corona nchini kuanzisha mashambulizi katika baadhi ya maeneo ya nchi.