Kuongezeka mirengo ya Wayemeni wanaoilaumu na kuikosoa Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60822-kuongezeka_mirengo_ya_wayemeni_wanaoilaumu_na_kuikosoa_saudia
Matukio yanayojiri kusini mwa Yemen, vita vinavyoendelea na vile vile kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu nchini humo vimeifanya Saudi Arabia iandamwe kwa wakati mmoja na lawama na ukosoaji wa kila upande wa serikali ya Yemen iliyojiuzulu na ile ya Uokovu wa Kitaifa ya nchi hiyo.
(last modified 2026-09-10T06:05:36+00:00 )
May 06, 2020 20:11 UTC
  • Kuongezeka mirengo ya Wayemeni wanaoilaumu na kuikosoa Saudia

Matukio yanayojiri kusini mwa Yemen, vita vinavyoendelea na vile vile kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu nchini humo vimeifanya Saudi Arabia iandamwe kwa wakati mmoja na lawama na ukosoaji wa kila upande wa serikali ya Yemen iliyojiuzulu na ile ya Uokovu wa Kitaifa ya nchi hiyo.

Saudia imekuwa ikikabiliwa na matatizo ya pande kadhaa nchini Yemen. Baada ya kupita miaka mitano, vita ilivyoanzisha Riyadh dhidi ya Yemen bado havijamalizika huku hali ya nchi hiyo katika vita hivyo ikizidi kuwa mbaya. Jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi vimeimarisha zaidi nguvu na uwezo wao katika ulinzi wa anga na wa ndege zisizo na rubani na kuwa tishio kubwa kwa Saudia endapo itaamua kuendeleza vita dhidi ya nchi hiyo.

Kwa upande mwingine, mivutano na tofauti za ndani ya muungano wa kijeshi ulioivamia Yemen zimeshtadi, kiasi kwamba si Saudia na Imarati tu zinazotafautiana vikali, lakini Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen na serikali iliyojiuzulu ya Abdrabbuh Mansur Hadi nazo pia zinavutana vikali kufika hadi ya Baraza la Mpito kujitangazia mamlaka ya kujiendeshea mambo yake na kugeuka kuwa mshindani na mpinzani mkubwa wa serikali hiyo iliyojiuzulu.

Abdrabbuh Mansur Hadi (kulia) na Bin Salman

Kutokana na kujitokeza hali hiyo, lawama na ukosoaji wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen na baadhi ya maafisa wa serikali ya nchi hiyo iliyojiuzulu dhidi ya Saudia nao pia umeongezeka.

Ukosoaji wa viongozi wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa kwa mwenendo wa Saudia unatokana na hali kadhaa. Kwa upande mmoja, utawala wa Aal Saud ungali unaendeleza vita dhidi ya Yemen huku ukiwa hauheshimu usitishaji vita uliotangaza kuwa utautekeleza. Na kwa upande mwingine, Riyadh inaendelea kuandamwa na ukosoaji mkali wa viongozi wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa kutokana na inavyoendelea kuharibu miundomsingi ya Yemen na kuifanya hali ya maafa ya kibinadamu inayoshuhudiwa nchini humo izidi kuwa mbaya.

Kuhusiana na suala hilo, balozi wa Yemen mjini Tehran Sayyid Ibrahim ad-Dailami amelieleza shirika la habari la Iran Press kuwa, Saudia haina dhamira na nia ya dhati ya kuhitimisha vita dhidi ya Yemen. Sababu ni kwamba kushindwa katika vita vya Yemen kutaathiri hali ya ndani ya Saudia ikiwemo taathira ya vita hivyo kwa nafasi ya Riyadh nchini Yemen na pia taathira yake kwa nafasi ya Mohammad bin Salman kwa ajili ya kukalia kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.

Sayyid Ibrahim ad-Dailami, balozi wa Yemen mjini Tehran

Vita ilivyoanzisha Saudia dhidi ya Yemen vimeharibu zaidi ya asilimia 80 ya miundomsingi ya nchi hiyo na kusababisha pia maafa ya kibinadamu hususan katika sekta za afya na lishe, ambayo yamechangiwa pia na sera mbovu za utawala wa zaidi ya miongo miwili wa Ali Abdullah Saleh ambao umeiweka Yemen kwenye kundi la nchi masikini zaidi za Kiarabu.

Kutokana na athari za vita vya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia, hivi sasa Wayemeni zaidi ya milioni 22 kati ya watu wote milioni 24 wa nchi hiyo wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Balozi wa Yemen mjini Tehran amegusia pia nukta hiyo na kueleza kwamba, hali ni mbaya sana katika sekta mbali mbali zikiwemo za uchumi, hali ya maisha ya watu na afya kutokana na athari hasi za vita.

Lakini mbali na ukosoaji wa maafisa wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa, baadhi ya viongozi wa serikali ya Yemen iliyojiuzulu, nao pia wamejiunga tena na safu ya wakosoaji wa utawala wa Aal Saud waksisitiza kuwa, mwenendo na muamala wa Saudia ndio uliosababisha Baraza la Mpito lishike hatamu za madaraka kusini mwa Yemen.

Mnamo mwezi uliopita wa Aprili, Baraza la Mpito la Kusini lilijitangazia mamlaka ya kujiendeshea mambo yake baada ya kuituhumu serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi kuwa uendeshaji wake wa mambo ni mbovu na haina ufanisi katika utendaji.

Ahmed bin Ahmed al-Maisari, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen anaitakidi kuwa, kimya cha Saudia kwa hatua zilizochukuliwa na Baraza la Mpito katika miji ya Socotra na Aden na ambazo zinaungwa mkono na Imarati ndiyo sababu kuu iliyochochea uamuzi uliochukuliwa karibuni na baraza hilo.

Ahmed bin Ahmed al-Maisari

Al-Maisari anaeleza pia kwamba, kabla ya mwezi wa Ramadhani, Saudia ilimtaka Mansur Hadi aakhirishe zoezi la kuingiza jeshi lake mjini Aden. Mansur Hadi hakuliafiki wazo hilo lakini alikubali shingo upande kutekeleza takwa hilo la Riyadh. 

Anavyoamini Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali ya Yemen iliyojiuzulu, katika hatua iliyochukuliwa na Baraza la Mpito la Kusini ya kujitangazia mamlaka ya kujiendeshea mambo yake, Saudia ilikuwa shauri moja na Imarati na ilichofanya ni kuipatia fursa na upendeleo Abu Dhabi.

Kwa ujumla na mazingira yalivyo yanaonyesha kuwa, kuendeleza vita dhidi ya Yemen si tu hakutainufaisha Saudi Arabia lakini pia kutauzidishia utawala wa Aal Saud matatizo ya ndani na ya kieneo.../