Umoja wa Mataifa wakaribisha na kupongeza kuundwa serikali mpya nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60852-umoja_wa_mataifa_wakaribisha_na_kupongeza_kuundwa_serikali_mpya_nchini_iraq
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha kwa mikono miwili na kupongeza kuundwa serikali mpya ya Iraq na kusisitiza juu ya kushirikishwa makundi yote katika mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2020 06:52 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakaribisha na kupongeza kuundwa serikali mpya nchini Iraq

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha kwa mikono miwili na kupongeza kuundwa serikali mpya ya Iraq na kusisitiza juu ya kushirikishwa makundi yote katika mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo.

Antonio Guterres amesisitiza kuwa, anaiunga mkono serikali mpya ya Iraq inayoongozwa na Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi na ameitaka serikali hiyo ifanye marekebishesho ya kimsingi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi sambamba na kuimarisha asasi za kidemokrasia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, serikali mpya ya Iraq inapaswa kuzingatia maslahi ya Wairaqi wote iwe ni vijana, wake kwa waume, matabaka yote ya jamii ikiwemo jamii ya waliowachache.

Kadhalika Antonio Guterres ameeleza kuwa, Umoja wa Mataifa unawaunga mkono wananchi na serikali ya Iraq katika juhudi zake za kukabiliana na virusi vya Corona na kufikiwa malengo ya nchi hiyo ya ustawi na maendeleo.

Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq

Hatimaye juzi baada ya miezi mitano ya mkwamo wa kisiasa nchini Iraq, Bunge la Iraq liliidhinisha Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi baada ya kulipigia kura ya kuwa na imani nalo.

Baada ya serikali ya Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi kuridhiwa na Bunge la Iraq, kivitendo kipindi cha muda cha serikali ya mshikizo ya Adil Abdul-Mahdi nacho kimefikia tamati na mkwamo wa kisiasa wa nchi hiyo uliodumu kwa miezi mitano nao takribani umemalizika.

Serikali mpya ya Iraq inakabiliwa na changamoto nyingi likiwemo suala la kurejesha usalama na kuboresha maisha ya wananchi wa nchi hiyo ambayo yamevurugika hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Corona.