Jihadul Islami: Haki ya taifa la Palestina si ya kupigwa mnada
Harakati ya Muqawama ya Jihadul-Islami ya Palestina imesema kwamba, haki ya taifa la Palestina si ya kupigwa mnada wala kutolewa zawadi na kwamba na njia pekee ya kufikia usalama, ni kuondoka wavamizi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina.
Harakati ya Jihadul-Islami imetoa taarifa hiyo kwa mnasaba wa siku ya 'Nakba' na imesema kwamba, kwa mazingira yoyote yale taifa la Palestina kamwe halitozembea msimamo wake kuhusiana na haki yake iliyoporwa na Wazayuni. Katika taarifa hiyo kumesisitizwa kwamba ardhi za Palestina kuanzia bahari hadi mto, ni haki halisi ya Wapalestina na amefafanua kwamba chaguo la muqawama wa kupambana kwa kutumia silaha, ni chaguo bora zaidi kwa ajili ya kuwakabili wavamizi wa Kizayuni.
Tarehe 14 Mei 2020 ilisadifiana na mwaka 72 za kuondolewa mamia ya maelfu ya Wapalestina katika ardhi zao asilia na kufanywa wakimbizi. Aidha tarehe 15 Mei 2020 imesadifiana na mwaka wa 72 wa kuundwa utawala haramu na pandikizi wa Israel katika ardhi walizoporwa Wapalestina. Kufuatia hali hiyo, kila inapofikia tarehe 15 Mei kila mwaka, raia wa Palestina huwa wanafanya maandamano ya kukumbuka 'Siku ya Nakba' ulipoundwa utawala katili wa Kizayuni ndani ya ardhi zao.