Mapambano ni njia pekee ya Wapalestina kujibu jinai za Wazayuni
Huku Siku ya Kimataifa ya Quds ikikaribia, Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Ghaza wamefanya maandamano na kusisitiza kwamba mapambano na muqawama wa pande zote ndio njia pekee ya kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mahir Mazhar, kiongozi wa Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina siku ya Jumatatu alishiriki katika maandamano ya Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuhusu muqawama wa pande zote katika kukabilaina na njama za Israel dhidi ya taifa la Palestina.
Mahir Mazhar amepinga hatua yoyote ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na kusema, hakuna mtu yeyote anayeweza kuakhirisha au kupuuza haki ya Wapalestina ya kurejea katika ardhi zao za jadi.
Kiongozi wa Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina amesema kuna udharura wa kuwepo umoja na mshikamano wa Wapalestina kwa ajili ya maslahi ya kitaifa.
Amesema mshikamano ni njia ya kuunda nguvu za kisiasa za wananchi na uongozi shupavu kwa ajili ya kukabiliana na njama za maghasibu ikiwa ni pamoja na mpango wa Marekani-Kizayuni wa 'Muamala wa Karne'.