Ndege za kivita za muungano wa Saudia zaendeleza mashambulizi Yemen
Ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudi Arabia zimeendelea kushambulia maeneo ya Yemen na hivyo kukiuka madai ya usitishwaji vita wa muda wa muugano huo.
Kwa mujibu wa taarifa, ndege za kivita za Saudia zimetekeleza mashambulizi katika maeneo kadhaa ya mkoa wa Hajjah kaskazini magharibi mwa Yemen.
Aidha ndege hizo za kivita za muungano wa Saudia zimeuhujumu mkoa wa Al Hudayda mara 51 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
Kwingineko jana pia ndege za kivita za Saudia zilidondosha mabomu katika maeneo ya raia mkoani Saada.
Muungano vamizi wa Saudia mnamo Aprili 9 ulitangaza kuwa utasitisha kwa muda vita dhidi ya Yemen kwa lengo la kusaidia jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 katika nchi hiyo. Hata hivyo masaa machache tu baada ya tangazo hilo, muungano huo ulitekeleza mashambulizi kadhaa dhidi ya Yemen.
Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.
Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia.