Familia: Mpalestina aliyeuawa na jeshi la Israel alikuwa mlemavu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i61325-familia_mpalestina_aliyeuawa_na_jeshi_la_israel_alikuwa_mlemavu
Kijana wa Kipalestina aliyeuawa jana Jumamosi na wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kupigwa risasi katika mji mtakatifu wa Quds alikuwa mlemavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 31, 2020 06:58 UTC
  • Familia: Mpalestina aliyeuawa na jeshi la Israel alikuwa mlemavu

Kijana wa Kipalestina aliyeuawa jana Jumamosi na wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kupigwa risasi katika mji mtakatifu wa Quds alikuwa mlemavu.

Hayo ni kwa mujibu wa familia ya kijana huyo anayeitwa Iyad el-Hallak aliyekuwa na umri wa miaka 32, na aliyekuwa na ugonjwa wa usonji (autism). Mama mzazi wa kijana huyo anayefahamika kama Rana amesema mwanawe huyo aliuawa kikatili na askari wa Israel jana asubuhi akienda katika shule ya walemavu ambako anafanya kazi.

Msemaji wa polisi ya utawala haramu wa Israel, Micky Rosenfeld amedai kuwa, askari polisi wa utawala huo pandikizi walimiminia risasi mlemavu huyo wakidhani kuwa alikuwa amebeba bastola. Hata hivyo mashuhuda na watu wa familia ya kijana huyo wamekadhibisha madai kuwa kijana huyo alikuwa na silaha ya moto wakati wa kuuawa kwake.

Mauaji hayo ya kikatili ya kijana wa Kipalestina mwenye ulemavu yameibua ghadhabu na hasira kali ndani na nje ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Askari katili wa Israel katika mji mtakatifu wa Quds

Kwenye mitandao ya kijamii, mauaji hayo ya kikatili yamefananishwa na mauaji ya kibaguzi yaliyofanywa na polisi ya Marekani hivi karibuni dhidi ya Mmarekani mweusi.

Kijana mwingine wa Kipalestina aliuawa juzi kwa kupigwa risasi na askari usalama wa Israel karibu na kitongoji cha Halamish huko kaskazini magharibi mwa Ramallah, huo ukiwa ni muendelezo wa ukatili wa maafisa usalama wa Israel dhidi ya Wapalestina.