Tamim: Wakati umefika wa kuweka wazi uhusiano wa Israel na Waarabu
(last modified Mon, 08 Jun 2020 02:35:50 GMT )
Jun 08, 2020 02:35 UTC
  • Tamim: Wakati umefika wa kuweka wazi uhusiano wa Israel na Waarabu

Mkuu wa zamani wa Jeshi la Polisi la Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu ameibua mijadala na wimbi la malalamiko baada ya kutoa mwito kwa nchi za Kiarabu kuufanya wa kawaida uhusiano wao na utawala haramu wa Israel.

Dhahi Khalfan Tamim amesema mataifa ya Ghuba ya Uajemi na ulimwengu wa Kiarabu yanapaswa kukiri kuwa yapo mbioni kuimarisha uhusiano wao na Tel Aviv.

Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, afisa huyo wa zamani wa ngazi ya juu wa Jeshi la Polisi mjini Dubai huko Imarati ameeleza bayana kuwa, "ukweli ni kwamba, haina maana yoyote kutoitambua Israel."

Ameenda mbali zaidi na kuusifu utawala huo pandikizi unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kudai kuwa "umejengeka katika misingi ya sayansi, elimu, mafanikio na uhusiano thabiti na nchi zote zinazostawi."

Imarati imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha uhusiano wake na Israel

Amekariri madai yake ya huko nyuma kwamba Qatar inaunga mkono ugaidi na kudai kuwa,"mara tu mataifa ya Ghuba ya Uajemi yatakapoufanya wa kawaida uhusiano wao na Israel, nafasi ya Qatar ya kuunga mkono mashirika ya kigaidi itafikia ukingoni."

Mkuu huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi la Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu ambaye amekuwa akitoa kauli tatanishi amewahi kunukuliwa na televisheni ya al-Alam akisema kuwa, Imarati haiwezi kuwasaidia Wapalestina wa Ukanda wa Gaza madhali bado Harakati ya Mapambano ya Kiislamu HAMAS iko katika ukanda huo.