Stratijia ya Hamas kwa ajili ya kukabiliana na Israel
Mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ametangaza stratijia yenye nguzo nne kwa ajili ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel
Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuzindua mpango wake wa kibaguzi na habithi uliopewa jina la Muamala wa Karne hapo tarehe 28 Januari mwaka huu, utawala wa Kizayuni wa Israel ulianza kuweka wazi zaidi sera zake za kimabavu na kutaka kutwaa ardhi zaidi za Palestina. Katika mkondo huo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kiongozi wa chama cha Bluu na Nyeupe, Benny Gantz ambao wameunda serikali ya mseto, mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu walifikia makubaliano ya kutwaa ardhi ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi na kuiunganisha na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Imepangwa kuwa mpango huo utatekelezwa rasmi tarehe Mosi Julai.
Makundi na harakati za mapambano ya ukombozi za Palestina yamepinga vikali mpango huo wa kibaguzi na kutoa mapendekezo kadhaa ya kukabiliana nao. Hata hivyo inaonekana kuwa, stratijia yenye vipengee vinne iliyopendekezwa na Ismail Hania ndiyo mpango kamili zaidi kwa ajili ya kukabiliana utawala wa Kizayuni.
Awamu ya kwanza ya stratijia hiyo ni kujiondoa katika makubaliano ya Oslo na kukomesha kabisa utekelezaji wa majukumu yaliyoainishwa katika makubaliano hayo.
Pendekezo hili lilikuwa tayari limetolewa na badhi ya viongozi wa Palestina akiwemo Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas. Kukataliwa kwa Muamala wa Karne na mpango wa kutwaa ardhi ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi vimevuruga kabisa mipango ya Washington na Tel Aviv na hapana shaka kuwa, kujiondoa katika makubaliano ya Oslo kutahitimisha kabisa njama hizo.
Awamu ya pili ya mapendekezo ya Hamas ni kuanzisha mapambano ya pande zote ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuimarisha harakati za upinzani za wananchi, vyombo vya habari, mapambano ya kisiasa na kiuchumi na zaidi mapambano ya silaha. Hii ni kwa sababu kama kutapatikana makubaliano ya kujiondoa katika mapatano ya Oslo, basi kutakuwepo udharura wa kuimarisha zaidi mapambano dhidi ya Wazayuni maghasibu. Wakati huo huo utawala wa Kizayuni umeonyesha kuwa, hauwezi kuhimili vishindo vya mapambano ya silaha. Mapambano ya silaha katika mazingira ya sasa yanaweza kuwa jibu halisi kwa Muamala wa Karne wa Donald Trump kwa sababu moja kati ya vipengee muhimu vya mpango huo ni kuwapokonya silaha wanaharakati na makundi ya ukombozi ya Palestina.
Nguzo ya tatu ya mpango wa Ismail Hania ni kufikiwa makubaliano juu ya suala la kutazama upya muundo wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) kwa njia ambayo itajumuisha pamoja makundi na harakati zote za kitaifa na kiislamu za Palestina. Stratijia hii itakuwa na maana ya kuwa na mtazamo wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina. Kama litakubaliwa, pendekezo hili linaweza kuwa pigo kubwa kwa mpango habithi wa Muamala wa Karne.
Nguzo ya nne ya pendekezo la Mkuu wa Idara ya Siasa ya Hamas ni kuanzishwa muungano wa kikanda katika upeo wa Kiarabu na Kiislamu kwa ajili ya kuitetea Palestina. Kwa hakika awamu hii inapaswa kutekelezwa na pande zisizo za Kipalestina japokuwa inaonekana kuwa utekelezaji wake utakuwa mgumu sana kutokana na ukweli kwamba, baadhi ya nchi za Kiarabu kama Saudi Arabia zinafanya jitihada za kuanzisha uhusiano wa waziwazi na utawala ghasibu na unaoendelea kuua Wapalestina na zinashirikiana na Marekani katika kutelekeza mpango habithi wa Muamala wa Karne.
Hata hivyo inatupasa kusisitiza kuwa, hakuna udharura muungano huo wa kikanda kwa ajili ya kuitetea Palestina uundwe na nchi za Kiarabu bali nchi za Kiislamu na za kimapinduzi zinazopinga ubeberu, dhulma na uonevu zinaweza kusimama katika safu moja katika muungano huo na kuwatetea Wapalestina.