Hamas yapongeza ujumbe wa Ayatullah Khamenei, yaahidi kudumisha mapambano
(last modified Tue, 07 Jul 2020 02:31:07 GMT )
Jul 07, 2020 02:31 UTC
  • Hamas yapongeza ujumbe wa Ayatullah Khamenei, yaahidi kudumisha mapambano

Mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amepongeza majibu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei kwa barua ya Mkuu wa Idara ya Siasa ya harakati hiyo na kusema: Taifa la Palestina litadumisha mapambano hadi litakaposhinda na kuvunjilia mbali mipango ya kughusubu eneo la Ukingo wa Magharibi.

Ismail Ridhwan amesema kuwa, jibu la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, kwa barua ya Mkuu wa Idara ya Siasa ya Hamas, Ismail Haniya, linaakisi himaya na uungaji mkono wa kistratijia wa Iran kwa taifa la Palestina na mapambano yao.

Ridhwan ameongeza kuwa himaya na misaada ya Iran kwa watu wa Palestina vina taathira ya moja kwa moja katika mapambano ya kukabiliana na uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel.

Katika barua yake ya jana kwa Mkuu wa Iidara ya Siasa ya Hamas, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwasaidia na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na kuvunja shari ya utawala bandia na ghasibu wa Israeli. 

Ayatullah Khamenei

Ayatullah Khamenei amesisitiza udharura wa kuwa macho na kudumishwa umoja na mshikamano wa wananchi na harakati za Palestina ili kuzima njama chafu za adui na akakumbusha kuwa: Kama ilivyokuwa huko nyuma na kwa kuzingatia wajibu wake wa kidini na kiutu na uliosimama juu ya misingi ya thamani za Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasita kufanya jitihada kubwa za kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina, kupigania haki zao na vilevile kuvunja na kuzima shari ya utawala bandia na ghasibu wa Israel.  

Tags