Rais wa Lebanon: Tutawapa adhabu kali waliosababisha kutokea mripuko wa Beirut
Rais Michel Aoun wa Lebanon amesisitiza ulazima wa kufanyika uchunguzi haraka iwezekanavyo ili kubaini nini hasa kilichotokea kuhusiana na tukio la mripuko wa Jumanne katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut.
Akihutubia kikao cha baraza la mawaziri jana Jumatano, Rais Aoun aliashiria mripuko uliotokea juzi katika bandari ya Beirut, ambapo sambamba na kupongeza juhudi za vyombo vya usalama na timu za utabibu za nchi hiyo alisema, waliosababisha kutokea mripuko huo watapewa adhabu kali kabisa.
Kwa mujibu wa Aoun tani 2,750 za mada za amoniamu naitreti zinazotumika kwa utengenezaji wa mbolea na mabomu zilikuwa zimehifadhiwa katika bandari ya Beirut kwa muda wa miaka sita bila kuchukuliwa tahadhari za kiusalama.
Rais wa Lebanon vilevile ameitaka Idara Kuu ya utoaji huduma za misaada ya kibinadamu ya nchi hiyo kuchukua hatua ya kusawazisha na kurekebisha uharibifu uliotokea na kutoa huduma na misaada inayohitajika.
Katika kikao hicho cha baraza la mawziri, Waziri Mkuu Hassan Diyab alisema, yaliyotokea Lebanon ni pigo kubwa, kwa sababu hiyo matokeo ya uchunguzi inapasa yajulikane haraka.
Diyab ameeleza kwamba, kutokana na tukio hilo, huu ni wakati wa raia wa nchi hiyo kuthibitisha Ulebanon wao na akavitaka vyama vya siasa viweke kando tofauti zao katika mazingira hayo hasasi na kulikabili janga lililotokea.
Meya wa jiji la Beirut Jamal Itani amesema yaliyotokea siku ya Jumanne ni balaa kwa Beirut na Lebanon nzima.
Gavana wa jiji hilo Marwan Abboud amesema, watu wapatao laki tatu wamebaki bila makazi huku hasara iliyosababishwa na mripuko huo ikikadiriwa kuwa ni kati ya dola bilioni tatu hadi tano.
Wakati huohuo ripoti kutoka Beirut zinaeleza kuwa baraza la mawaziri limeamuru maafisa wa bandari ya Beirut waweke kwenye kizuizi cha nyumbani ili kupisha uchunguzi wa tukio la mripuko wa siku ya Jumanne uliosababisha watu wasiopungua 100 kuuawa na wengine 4,000 kujeruhiwa huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka.../