Makundi ya Muqawama Iraq: Wamarekani wasipoondoka, hawatosalimika na mashambulio yetu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i62935-makundi_ya_muqawama_iraq_wamarekani_wasipoondoka_hawatosalimika_na_mashambulio_yetu
Makundi ya muqawama ya Iraq yamesisitiza ulazima wa wanajeshi wa Marekani kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo na kuonya kuwa, ikiwa hilo halitofanyika, yataanzisha makabiliano ya kijeshi dhidi yao.
(last modified 2026-02-15T05:39:07+00:00 )
Aug 21, 2020 08:14 UTC
  • Makundi ya Muqawama Iraq: Wamarekani wasipoondoka, hawatosalimika na mashambulio yetu

Makundi ya muqawama ya Iraq yamesisitiza ulazima wa wanajeshi wa Marekani kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo na kuonya kuwa, ikiwa hilo halitofanyika, yataanzisha makabiliano ya kijeshi dhidi yao.

Makundi ya muqawama nchini Iraq yamesisitiza katika taarifa yao: "Tulitarajia Waziri Mkuu Mustafa al Kadhimi, atakuwa kama alivyoahidi, mwakilishi wa taifa lenye ghera la Iraq kwa ajili ya kudhamini mamlaka ya kujitawala; na si rais wa Marekani Donald Trump kuwa mtu wa kumuainishia yeye maagizo ya kutekeleza".

Taarifa hiyo imeeleza bayana kwamba, baadhi ya mipango itakayopelekwa Iraq na al Kadhimi kutoka Washington ina sura ya kipropaganda na kutaka kuhadaa watu; na baadhi yao ni kwa ajili ya wizi, uporaji, ukoloni na kurejesha upya ukiritimba wa Marekani ndani ya Iraq.

Makundi ya muqawama nchini Iraq yametangaza kuwa, kutojadiliwa suala la kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini nchini Iraq katika safari ya al Kadhimi huko Washington kunamaanisha kwamba Waziri Mkuu  wa Iraq ameyakhalifu mamlaka ya utawala, heshima ya taifa na katiba ya nchi hiyo.

Trump na Al Kadhimi

Taarifa ya makundi hayo imeeleza kinagaubaga kuwa, endapo hautafikiwa mwafaka kuhusu kuondoka kikamilifu Marekani nchini Iraq, makundi ya muqawama yatakuwa na haki kisheria na kidini kuivuka awamu ya muqawama wa hatua kwa hatua na utoaji fursa ya mazungumzo ya kisiasa, na kuingia kwenye awamu ya makabiliano na mashambulio dhidi ya maslahi yote ya Marekani.

Siku ya Jumanne iliyopita, Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al kadhimi alielekea Marekani kwa mazungumzo na rais wa nchi hiyo Donald Trump. Katika mazungumzo yake na Al Kadhimi, Trump alidai kwamba Marekani itawaondoa askari wake huko Iraq ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Itakumbukwa kuwa tarehe 5 Januari mwaka huu, bunge la Iraq lilipitisha mswada wa kutaka askari vamizi wa Marekani waondoke katika ardhi ya nchi hiyo.../