Sheikh Naim Qassim: Hizbullah haitoruhusu Israel iivamie Lebanon
Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, harakati hiyo ya Kiislamu kamwe haitoiruhusu Israel na waungaji mkono wake waivamie tena Lebanon.
Mtandao wa habari wa al Ahd wa Lebanon umemnukuu Sheikh Naim Qassim akisema hayo usiku wa kuamkia leo mjini Beirut na kuongeza kuwa, Hizbullah ya Lebanon haitokubali kuburuzwa na watu wenye nia ya kufifiliza heshima na ushindi wa muqawama.
Amma kuhusiana na kuundwa serikali mpya nchini Lebanon, Sheikh Naim Qassim amesema, Hizbullah inataka Lebanon iwe na serikali yenye nguvu, inayoshirikisha pande zote na iliyoundwa kwa mujibu wa katiba.
Naibu huyo wa Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amekanusha madai ya uongo yaliyotolewa dhidi ya harakati hiyo kuhusu kujilimbikizia silaha katika bandari ya Beirut na kuongeza kuwa, wanaoeneza uvumi huo wana nia ya kufifiliza mafanikizo ya harakati hiyo ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel na kulinda usalama na umoja wa ardhi ya Lebanon lakini tuhuma zote hizo zinawarejea hao hao wanaozitoa ambao imethibitika kuwa ndio waliosababisha kutokea mripuko mkukbwa katika bandari ya Beirut.
Mripuko mkubwa uliotokea siku ya Jumanne katika bandari ya Beirut umesababisha vifo vya watu wasiopungua 157 na kujeruhi karibu wengine elfu tano.