Ansarullah yataka kuundwa muungano wa Kiislamu wa kupinga uhusiano na Israel
Msemaji wa harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah ametoa wito wa kuundwa muungano wa Kiislamu dhidi ya hatua yoyote ya kuanzishwa uhusiano baina ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel.
Mohammed Abdul-Salam ameashiria hatua ya serikali ya Bahrain ya kuamua kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: Kwa mwelekeo wake wa sasa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imethibitisha kuwa ni mlinzi wa maslahi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la magharibi mwa Asia.
Abdul-Salam amesema kuwa taifa la Yemen linapinga katakata msimamo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wa kubariki suala la kuanzishwa uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na amekosoa vikali nafasi ya jumuiya hiyo katika mchakato wa kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Bahrain na utawala huo haramu.
Jumatano iliyopita Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilitupilia mbali muswada uliowasilishwa na Palestina wa kulaaniwa makubaliano ya kuanzishwa uhusiano baina ya Imarati na utawala ghasibu wa Israel.
Ofisi ya harakati ya Ansarullah nchini Yemen pia imesema kuwa tawala zinazoanzisha uhusiano na utawala unaoendelea kuua watoto wa Palestina haziwakilishi mataifa yao na kusisitiza kuwa: Bahrain ni utawala kibaraka wa Marekani na Israel na sasa imetangaza waziwazi kujiunga na garimoshi la kuwa na uhusiano na Wazayuni.
Ikumbukwe kuwa utawala wa Bahrain umechukua hatua ya kusaliti malengo matukufu ya Palestina na Ulimwengu wa Kiislamu kwa kuamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, ukiwa umepita mwezi mmoja tu tangu Imarati pia kuchukua hatua kama hiyo ambayo imekosolewa vikali na kulaaniwa na makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani..