Ayatullah Sistani aunga mkono uchaguzi wa mapema wa Bunge nchinI Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63408-ayatullah_sistani_aunga_mkono_uchaguzi_wa_mapema_wa_bunge_nchini_iraq
Kiongozi mkuu wa kidini wa Iraq ametangaza uungaji mkono wake kwa uchaguzi wa mapema wa bunge ambao ni miongoni mwa matakwa muhimu ya waandamanaji ambao wanaendelea kufanya maandamano kwa miezi kadhaa sasa tangu mwaka jana dhidi ya ufisadi na hali mbaya ya uchumi nchini Iraq.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 14, 2020 02:42 UTC
  • Ayatullah Sistani aunga mkono uchaguzi wa mapema wa Bunge nchinI Iraq

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iraq ametangaza uungaji mkono wake kwa uchaguzi wa mapema wa bunge ambao ni miongoni mwa matakwa muhimu ya waandamanaji ambao wanaendelea kufanya maandamano kwa miezi kadhaa sasa tangu mwaka jana dhidi ya ufisadi na hali mbaya ya uchumi nchini Iraq.

Ayatullah Sistani ametangaza msimamo huo katika mazungumzo yake na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Jeanine Hennis-Plasschaert yaliyofanyika jana Jumapili katika mji mtakatifu wa Najaf.

Amesema uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika mwaka ujao una umuhimu mkubwa, na kuongeza kuwa: Wairaq wanapaswa kuhimizwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, akionya kuwa kutofanyika uchaguzi kama ilivyopangwa au kwa njia huru na ya haki kutatishia umoja na mustakabali wa watu wa Iraq.

Kwa upande wake, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, iwapo uchaguzi huo wa mapema wa Bunge la Iraq utafanyika kwa njia sahihi na za kuaminika, unaweza kufungua ukurasa muhimu kwa nchi hiyo.

Tarehe 24 Disemba mwaka jana Bunge la Iraq liliidhinisha sheria mpya ya uchaguzi ambayo inaruhusu wapiga kura kuchagua wabunge mmoja mmoja badala ya kuchagua kutoka orodha za vyama.

Uchaguzi huo unatazamiwa kufanyika mapeka mwaka ujao.

Ayatullah Sistani mwenyewe amekuwa akiunga mkono uchaguzi wa mapema wa bunge ambao unaonekana kama hatua muhimu ya kusaidia juhudi za kumaliza matatizo yanayoisumbua nchi ya Iraq.