Saudia, Imarati, Israel; zashirikiana kuchochea machafuko nchini Iraq
Mbunge mmoja nchini Iraq amefichhua njama zinazofanywa na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na utawala wa Kizayuni wa Israel, za kuzusha machafuko nchini Iraq.
Shirika la habari la al Ma'aluma limeripoti habari hiyo na kumnukuu Abdul Amir Taiyan, mbunge wa mrengo wa al Swadiqun katika Bunge la Iraq akifichua hayo na kuongeza kuwa, Saudia, Imarati na utawala wa Kizayuni zinawachochea baadhi ya watu katika mji wa Nasiriyah ambao ni makao makuu ya mkoa wa Dhi Qar ili wazushe machafuko na wawashe moto mjini humo.
Amesema, matukio ya mji wa Nasiriyah na kuweko huko jela ya al Hut ambayo ndani yake mna wafungwa pia wa Saudi Arabia na Imarati, kumepelekea kuzuka wasiwasi mkubwa katika eneo hilo. Ameongeza kuwa, mamluki wa Saudia, Imarati na utawala wa Kizayuni wamemwaga fedha nyingi katika mji wa Nasiriyah na mkoa wa Dhi Qar kiujumla ili kuchochea machafuko na kuwasha moto mjini humo.
Itakumbukwa kuwa miji mbalimbali ya Iraq ukiwemo mji mkuu, Baghdad pamoja na Basra na Nasiriya imeshuhudia machafuko na maandamano ya kulalamikia ukosefu wa ajira na umaskini katika miezi ya hivi karibuni.
Baadhi ya wahalifu na wafanya machafuko walitumia vibaya maandamano ya wananchi kuwasha moto matairi ya gari jana Jumatatu mbele ya shirika la mafuta la Dhi Qar ili kuzuia wafanyakazi wasiingie kwenye ofisi za shirika hilo kwa ajili ya kufanya kazi zao.