Waziri Mkuu wa Lebanon ajiuzulu baada ya kushindwa kuunda serikali
Waziri Mkuu wa Lebanon, Mustapha Adib ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo, baada ya kushindwa kuunda serikali.
Adib ameshindwa kuunda kile alichokiita serikali ya kiteknokrati isiyoegemea mrengo wowote wa kisiasa katika hali ambayo, aliungwa mkono na mirengo ya ndani na ya nje nchi wakati wa uteuzi wake.
Mwanadiplomasia huyo ambaye alikuwa balozi wa Lebanon mjini Berlin amesema leo Jumamosi katika hotuba yake kwa taifa kuwa, "Najiuzulu kwa kushindwa kutekeleza jukumu nililotwikwa la kuunda serikali."
Vyanzo vya habari vimedokeza kuwa, Adib ambaye ametangaza kujiuzulu muda mfupi baada ya kukutana farghani na Rais Michel Aoun wa nchi hiyo, ameshindwa kuunda Baraza la Mawaziri hususan kuteua shakhsia ambaye angepewa Wizara ya Fedha.
Siku chache baada ya kujiri mlipuko mkubwa katika bandari ya Beirut na kusababisha karibu watu 200 kuuawa na wengine takribani 7,000 kujeruhiwa mwezi uliopita wa Agosti, aliyekuwa Waziri Mkuu Hassan Diab alitangaza kujiuzulu. Baada ya kujiuzulu Hassan Diab, tarehe 13 mwezi uliopita, Bunge la Lebanon lilipitisha kwa wingi wa kura jina la Mustapha Adib aliyekuwa amependekezwa na Rais Michel Aoun kushika wadhifa wa Waziri Mkuu.
Adib alikuwa na azma ya kuunda serikali ya wataalamu, ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kiuchumi na kifedha unaoikabili nchi hiyo ya Kirabu haraka iwezekanavyo.