Muqtada al-Sadr: Iraq si koloni la nchi ajinabi
Kiongozi wa Harakati ya Al-Sadr ya nchini Iraq amesema Wairaqi hawataruhusu nchi yao igeuzwe koloni la nchi yoyote ajinabi.
Sayyid Muqtada al-Sadr amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumamosi na kuongeza kuwa: Hatutaruhusu kuwa koloni la maajinabi, ima kwa nchi za mashariki au magharibi. Iraq ni nchi huru na yenye nguvu.
Ametoa mwito kwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo kuunda kamati ya kuchunguza wimbi la mashambulizi dhidi ya jumbe za kigeni na ofisi za kibalozi katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Sayyid Muqtada al-Sadr amesema bayana kuwa, mashambulizi hayo dhidi wanadiplomsia na ofisi za kibalozi mbali na kukiuka sheria, lakini pia yanatishia mamlaka ya serikali na mustakabali wa taifa hilo.
Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad na kambi za kijeshi za Marekani zimekuwa zikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni. Wananchi wa Iraq wanataka vikosi vamizi vya Marekani viondoke nchini humo haraka iwezekanavyo.
Kiongozi huyo wa kidini nchini Iraq amekuwa akisisitiza kuwa, lengo hasa la Washington kusalia nchini Iraq ni kulifanya taifa hilo lisalimu amri mbele ya Marekani na wala si kuikomboa nchi hiyo kutoka katika mikono na uvamizi wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).