Palestina; miongo miwili baada ya Intifadha ya Pili
Jumatatu ya jana tarehe 28 Septemba, ilisafidiana na kutimia miaka 20 tangu kulipotokea Intifadha ya Pili inayojulikana kama Intifadha ya al-Aqswa.
Hatua ya Ariel Sharon kiongozi wa wakati huo wa chama cha Likud na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa utawala ghasibu wa Israel ya kuuvunjia heshima msikiti wa al-Aqswa, iliandaa uwanja wa kuanza Intifadha ya al-Aqswa tarehe 28 Septemba mwaka 2000. Katika Intifadha hiyo iliyochukua muda wa miaka 5, Wapalestina wapatao 4,412 waliuawa shahidi na wengine takribani 49,000 walijeruhiwa. Aidha Waisrael wapatao1,100 waliangamizwa huku mamia miongoni mwao wakijeruhiwa.
Intifadha ya al-Aqswa ilianza katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umelazimika kuondoa majeshi yake kutoka kusini mwa Lebanon. Ukweli wa mambo ni kuwa, Israel ilifanya hujuma dhidi ya Msikiti wa al-Aqswa ili kufidia kushindwa kwake na muqawama wa Lebanon na kisha ukiliweka katika ajenda zake suala la kuanzisha vita dhidi ya Wapalestina. Nukta nyingine ni kuwa, Intifadha ya al-Aqswa ilianza katika mazingira ambayo, Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilikuwa imeutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel na mazungumzo ya mapatabno baina ya pande mbili yalikuwa yakiendelea.

Makubaliano ya Oslo baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel yalitiwa saini 1993 ambapo kwa mtazamo wa Nafiz Azzam, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina ni kuwa, baadhi waliyatambua makubaliano hayo kuwa yamebeba maana ya kufikia tamati muqawama na mapambano ya Palestina. Pamoja na hayo, moja ya matokeo muhimu ya Intifadha ya al-Aqswa yalikuwa ni kuimarika makundi ya muqawama huko Palestina.
Ukweli ni kuwa, Intifadha ya al-Aqswa sambamba na kuthibitisha kutokuwa na natija mwenendo wa mapatano na Israel, imeonyesha kuwa, mpambano na muqawama ni utendaji uliokubaliwa na wananchi wa Palestina. Katika uwanja huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilifanikiwa kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge wa mwaka 2005 na kisha ikaunda serikali.
Baada ya kupita miongo miwili tangu ilipoanza Intifadha ya al-Aqswa, hali ya Palestina ipo kwa namna ambayo kuna uwezekano wa kuanza Intifadha mpya. Gazeti la al-Qus al-Arabi limeandika katika moja ya ripoti zake kuhusiana na kadhia hii kwamba: Utawala wa Kizayuni wa Israel ungali unaendelea na ujenzi wake wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi sambamba na ukaliaji mabavu ardhi ya Palestina.

Mpango wa kibaguzi wa Muamala wa Karne ambao ulizinduliwa na serkali ya Marekani tarehe 28 Januari mwaka huu, ni upande wa pili wa jinai dhidi ya Palestina.
Upande wa tatu wa jinai hizi unapatikana katika kigezo kibaya na mkumbo wa baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel. Fauka ya hayo, Abdul-Nasser Farzanah, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti cha Kamati Maalumu ya Mateka na Wafungwa wa Kipalestina Walioachiliwa Huru ametangaza kuwa, tangu ilipoanza Intifadha ya al-Aqswa hadi sasa, Wapalestina 120,000 wametiwa mbaroni kwa tuhuma na visigizio hivi na vile ambapo 18,000 kati yao ni watoto wadogo na 2,000 ni wanawake.
Baada ya kupita miongo miwili tangu Intifadha ya al-Aqswa ilipoanza, sura halisi ya wafanya mapatano wa Kiarabu imedhihirika wazi kuliko wakati mwingine wowote ule.

Kumechorwa mstari batili juu ya mipango ya amani wa Marekani na imefahamika bayana kwamba, Washington si muungaji mkono wa amani tu, bali ni mtoa himaya na uungaji mkono kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel; utawala ambao hakubaliani hata chembe na mpango wa kuundwa serikali mbili katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kimsingi haukubaliani katu na suala la kuundwa dola huru la Palestina katika ardhi ya Palestina.
Asasi na jumuiya za kimataifa hususan Umoja wa Mataifa kimsingi zipo chini ya satwa na udhibiti wa Wazayuni na waungaji mkono wake na hazina ubavu wa kuchukua hatua yoyote ile ya kivitendo yenye lengo la kukomesha jinai za utawala ghasibu wa Israel. Hatimaye, muqawama umekubaliwa kuwa utendaji na njia ya mwisho ya kukabiliana na jinai za utawala haramu wa Israel.
Hivi sasa licha ya kuwa, watawala wa baadhi ya mataifa ya Kiarabu wametiliana saini makubaliano ya amani na Israel, lakini utawala huo ghasibu unakabiliwa na changamoto kemkemu ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ambapo kufanyika maandano ya kila wiki kwa muda wa miezi mitano mtawalia ni ishara ya wazi ya changamoto hizo.