Iraq; mwaka mmoja baada ya maandamano ya Oktoba Mosi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63768-iraq_mwaka_mmoja_baada_ya_maandamano_ya_oktoba_mosi
Oktoba Mosi mwaka uliopita, Iraq ilishuhudia maandamano makubwa ya watu yaliyogeuka na kuwa ya vurugu na hivyo kupelekea maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 02, 2020 07:33 UTC
  • Iraq; mwaka mmoja baada ya maandamano ya Oktoba Mosi

Oktoba Mosi mwaka uliopita, Iraq ilishuhudia maandamano makubwa ya watu yaliyogeuka na kuwa ya vurugu na hivyo kupelekea maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

Maandamano hayo yalichochewa na matatizo ya kimaisha na ufisadi katika serikali ya Iraq, lakini ghafla yalibadili mkondo na kuchukua sura ya ghasia, machafuko na mauaji ya raia kutokana na uingiliaji wa nchi za Magharibi na Kiarabu pamoja na magenge ya upotofu, waungaji mkono wa chama kilichopigwa marufu cha Baath na vilevile mabaki ya magaidi wa Daesh. Hatimaye maandamano hayo yalipelekea kujiuzulu Waziri Mkuu Adel Abdul Mahdi ambaye baada ya hapo aliiongoza Iraq kwa muda wa miezi mitano kama waziri msimamizi na hatimaye kuingia madarakani Mustafa al-Kadhimi kama waziri mkuu wa muda ambaye ataongoza nchi hadi wakati uchaguzi wa bunge utakapofanyika na kuundwa serikali mpya.

Swali muhimu la kujiiuliza hapa ni kwamba je, Iraq iko kwenye hali gani sasa baada ya kufanyika maandamano hayo mwaka uliopita?

Katika sekta ya uchumi, hali ya maisha ya watu wa nchi hiyo haijabadilika kwa sababu imeendeshwa kwa muda wa miezi mitano bila ya kuwa na serikali ya kudumu. Serikali ya Mustafa al-Kadhimi pia tokea ishike usukuani wa Iraq imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa za kisiasa na kiusalama, kama ambavyo imeshuhudia maandamano kadhaa ya wananchi na hasa katika mji wa Basra.

Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq

Katika uwanja wa siasa, matatizo ya Iraq yameongezeka maradufu. Hitilafu zilizojitokeza wakati wa kuarifishwa waziri mkuu mpya wa Iraq baada ya kujiuzulu Adel Abdul Mahdi, zimeongeza pengo na kuwatengenisha zaidi watu wa nchi hiyo. Suala hilo limewachochea wapinzani wa Iraq wapange njama ya kutaka kuipindua kijeshi serikali ya al-Kadhimi. Ukweli wa amambo ni kwamba baada ya kujiuzulu Adel Abdul Mahdi, umoja wa kisiasa nchini Iraq umekuwa ukidhoofika ambapo serikali ya al-Kadhimi inaendesha masuala ya nchi bila ya kuwa na uungaji mkono wa kutosha wa makundi muhimu ya kisasa.

Usalama wa taifa ndio ulioathirika zaidi kutokana na matukio ya maandamano ya mwezi Oktoba mwaka uliopita. Tukio muhimu zaidi likiwa ni la kuuawa shahidi, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq la Al-Hashdu-Sha'abi, ambao waliuawa kinyama na jeshi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad. Hatua hiyo ya serikali ya Marekani, ambao ni mfano wa wazi wa ugaidi unaodhaminiwa kiserikali, na pia ukiukaji wa wazi wa kujitawala Iraq, imezindua harakati mpya dhidi ya Marekani huko Iraq na pia kuzidisha mashinikizo dhidi ya serikali ya Baghdad.

Tarehe 5 Januari mwaka huu bunge la Iraq lilipitisha mswada wa kufukuzwa askari wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo ambapo mamilioni ya raia wa Iraq walifanya maandamano ya kuunga mkono jambo hilo na kuonyesha kuchukizwa kwao na Marekani. Wakati huohuo, baadhi ya makundi ya Iraq yameshambulia vituo vya kijeshi vya Marekani pamoja na ubalozi wa nchi hiyo nchini humo.

Mamilioni ya raia wa Iraq wakiandamana dhidi ya Marekani mjini Baghdad

Matokeo yake yamekuwa ni kuondolewa au kupunguzwa askari wa Marekani katika vituo hivyo na pia kufanyika mazungumzo mapya kati ya viongozi wa nchi mbili kuhusiana na hali ya askari wa Marekani walioko katika ardhi ya Iraq, mazungumzo ambayo hadi sasa hayajakuwa na natija ya wazi. Wakati huohuo, hivi karibuni kufuatia mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad, Washington imetishia kwamba itaufunga ubalozi wake huo, tishio ambalo inaonekana limetolewa kwa ajili tu ya kutoa mashinikizo dhidi ya serikali na makundi ya Iraq ili yatoe dhamana zaidi ya kulinda usalama wa wanajeshi wa Marekani walioko nchini humo.

Nukta ya mwisho ni kwamba, maandamano ya Oktoba Mosi mwaka uliopita na matukio yaliyofuatia, si tu kwamba hayajasaidia lolote katika kuboresha hali ya usalama nchini Iraq bali yameharibu zaidi hali ya mambo nchini humo. Shirika la habari la Euro News limeandika kuhusu suala hilo kwa kusema: 'Mwaka mmoja baada ya kufanyika maandamano hayo, wananchi ambao walimiminika mitaani kwa ajili ya kubadilisha hali ya mambo, sasa wanaamini kwamba hakuna lolote lililobadilika.'