Kushindwa Saudi Arabia kupata uanachama katika Baraza la Haki za Binadamu
Jitihada za Saudi Arabia za kuwa mwanachama tena wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa zimegonga ukuta baada ya kushindwa kupata kura zinazohitajika.
Katika zoezi la upigaji kura uliofanyika siku ya Jumanne tarehe 13 Agosti, Saudia ilipata kura 90 kati ya kura 193 wakati wa upigaji kura wa kujiunga na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, na hivyo kushindwa kupata tena uanachama katika taasisi hiyo. Kushindwa Saudia kupata uanachama tena wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kunatokana na faili jeusi la nchi hiyo katika kukiuka haki za binadamu ndani na nchi ya nchi hiyo.
uhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia ambaye katika miaka ya hivi karibuni amefanya mageuzi ya kimaonyesha akifanya hima na juhudi za kubadilisha sura ya nchi yake, amefanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamuu ndani ya nchi hiyo. Ukweli wa mambo ni kuwa, mageuzi yaliyofanywa na mrithi kijana Muhammad bin Salman hayakuwa ya kimsingi. Hii ni katika hali ambayo, ukiukaji wa haki za binadamu ni jambo la msingi ambalo lilipaswa kufanyiwa mageuzi.
Kutiwa mbaroni kiholea wanamfalme nchini Saudia hususan wanamfalme wanaoonekana kuwa tishio kama Muhammad bin Nayef na kamatakamata inayofanywa na utawala wa Aal Saud dhidi ya wanaharakati sambamba na ukandamizaji mkubwa dhidi ya raia ni mambo ambayo katika miaka ya hivi karibuni yamechukua mkondo wa kudhihirika wazi zaidi. Kwa msingi huo mageuzi ya kimaonyesho na ya kijuujuu ya bin Salman hayajawa na taathira yoyote ile.
Kuhusiana na jambo hilo, gazeti la The Guardian la nchini Uingereza limeashiria kushindwa Saudia juhudi zake za kuwa mwanachama tena wa Baraza la Haki za Binadamu na kuandika: Matokeo haya ni mithili ya dhoruba kali dhidi ya juhudi za Riyadh za kuboresha na kusafisha haiba na sura yake katika duru za kimataifa.
Katika uga wa masuala ya kigeni, Saudi Arabia ina sura mbaya na chafu zaidi katika ukiukkaji wa haki za binadamu. Mauaji ya Jamal Khashoggi mwandishi wa habari mtajika Msaudia wa gazeti la Washington Post la Marekani na vita vya takribani miaka sita dhidi ya Yemen ambayo ni maafa makubwa kabisa ya haki za binadamu yaliyowahi kushuhudiwa ulimwenguni katika miongo ya hivi karibuni ni sehemu ya faili jeusi la haki za binadamu la utawala wa Aal saud.
Katika miaka ya hivi karibuni utawala wa kifamilia wa Aal Saud umetumia gharama kubwa na kumwaga kitita kikubwa cha fedha ili kuzuia jina la Saudia lisiwekwe katika orodha nyeusi ya haki za binadamu. Hata hivyo, kuangukia pua Saudia katika uchaguzi wa Jumanne iliyopita wa Baraza la Haki za Binadamu, kumethibitisha kwamba, fedha ilizomwaga Riyadh hazijaisaidia kufikia malengo yake.
Yahya Asiri, Katibu Mkuu wa chama cha upinzani nchini Saudia cha Tajamu'u al-Watan ameandika katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter akitoa radiamali yake kwa kushindwa Saudia kupata tena uanachama katika Baraza la Haki za Binadamu: Saudia ilijitokeza kugombea nafasi hiyo ikidhani kwamba, kwa kutumia fedha inawezekana kufanya kila kitu, lakini katika zoezi la upigaji kura imeambulia kura chache zaidi za ndio, kutokana na kuwa na faili chafu la haki za binadamu.
Inaonekana kuwa, mbali na Saudia kuwa na faili jeusi la utendaji mbaya wa haki za binadamu, lakini kutokuweko Marekani katika baraza hilo ni sababu nyingine iliyopelekkea kuanguka Riyadh.
Mwaka 2018, Rais Donald Trump wa Marekani aliiondoa nchi yake katika Baraza la Haki za Binadamu akiituhumu taasisi hiyo ya kimataifa kwamba, eti inafanya mambo dhidi ya Israel. Kutokuweko Marekani sasa kumezifanya nchi wanachama kuwa huru katika kupiga kura na hivcyo kutofumbia macho faili jeusi la haki za binadamu la Saudia.
Nukta ya mwisho ni kuwa, kushindwa juhudi za Saudia za kuwa tena mwanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kumepongezwa na kupokewa kwa mikono miwili za asasi za kimataifa za haki za binadamu. Mara baada ya Saudia kushindwa, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch lilikaribisha hatua hiyo na kuandika katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Kufeli Saudia kupata kiti cha uanachama katika Baraza la Haki za Binadamu ni ushindi kwa wahanga wa mfumo huu wa ukandamizaji na hilo linakumbusha ulazima wa kuweko ushindani zaidi katika uchaguzi wa Umoja wa Mataifa.