Hamas: Imarati na Bahran ziipe Israel baadhi ya ardhi zao....
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kuwa kama watawala wa Imarati na Bahrain wanaliona suala la kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel ni jambo la kawaida basi watoe baadhi ya ardhi za nchi zao kwa utawala huo haramu.
Usama Hamdan ambaye ni miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa Hamas amesema kuwa, watawala wa Imarati na Bahrain wanaodai kuwa kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel kunadhamini maslahi ya nchi hizo wanapaswa kuelewa kwamba, utawala huo ghasibu unalinda maslahi yake tu na si maslahi ya nchi hizo.
Hamdani ameyasema hayo leo baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuwashutumu vikali wananchi wa Palestina na kudai kuwa hawana shukrani wala hawatambui fadhila, kutokana na kupinga hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Siku chache zilizopita pia balozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mjini Paris, Salman El Herfi aliliambia jarida la Ufaransa la Le Point kuwa, Imarati na Bahrain zimegeuka na kuwa Waisraeli hata kuwashinda Waisraeli wenyewe kwa hatua yao ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Tel Aviv.
Ulimwengu wa Kiislamu bali hata baadhi ya nchi zisizo za Waislamu kama Afrika Kusini zimeendelea kulaani kitendo cha kisaliti cha nchi za Bahrain na Imarati cha kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel unaoendelea kupora ardhi za Palestina na kuua kwa umati watu wa nchi hiyo.