Nov 02, 2020 04:22 UTC
  • Wapalestina 3 wauawa shahidi na jeshi katili la Israel

Vijana watatu wa Kipalestina wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la al-Jalil, kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Shirika la habari la IRNA limenukuu vyanzo vya habari vya Palestina vikiripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, watatu hao waliuawa jana Jumapili baada ya askari wa Kizayuni kuvamia makazi ya mmoja wa mateka wa Kipalestina katika mji wa Nablus anayefahamika kama Amjad Alawi, na kuanza kufyatua risasi ovyo.

Vile vile wanajeshi hao walishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani katika eneo la al-Arub, kaskazini mwa mji wa al-Khalil katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kadhalika wanajeshi wa utawala haramu wa Israel walivamia eneo la Az'im  ulioko mashariki mwa mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu, na kuwashambulia kwa risasi wakazi wa eneo hilo.

Katika miezi ya hivi karibuni, wananchi wa Palestina wameshadidisha maandamano ya kupinga mpango wa utawala pandikizi wa Israel wa kutaka kumega asilimia 30 ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuiunganisha na ardhi zingine za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu. 

Wapalestina katika maandamano ya kupinga kughusubiwa ardhi zao

Utawala huo wa Kizayuni unataka kutekeleza uporaji huo wa ardhi za Wapalestina katika hali ambayo, Imarati ilidai kuwa, lengo lake la kuanzisha uhusiano na Israel lilikuwa ni kuzuia utekelezaji wa mpango huo wa kulimega eneo la Ufukwe wa Magharibi.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu alikadhibisha madai ya kufutwa moja kwa moja mpango huo.

Tags