Sababu za kucheleweshwa kuundwa baraza jipya la mawaziri Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64451-sababu_za_kucheleweshwa_kuundwa_baraza_jipya_la_mawaziri_lebanon
Matarajio ya kuundwa baraza jipya la mawaziri nchini Lebanon yameambulia patupu baada ya zoezi hilo kuahirishwa. Ilitarajiwa kuwa, Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri angeunda baraza jipya la mawaziri katika siku chache zilizopita.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 05, 2020 23:02 UTC
  • Sababu za kucheleweshwa kuundwa baraza jipya la mawaziri Lebanon

Matarajio ya kuundwa baraza jipya la mawaziri nchini Lebanon yameambulia patupu baada ya zoezi hilo kuahirishwa. Ilitarajiwa kuwa, Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri angeunda baraza jipya la mawaziri katika siku chache zilizopita.

Kumetajwa sababu kuu mbili zilizopelekea kuahirishwa uundwaji wa baraza jipya la mawaziri la Lebanon. Kwanza ni kutetereka nafasi ya kisiasa ya Hariri na pili ni pendekezo lake la sura na muundo wa baraza jipya mawaziri. 

Saada Hariri ameteuliwa kuunda baraza la mawaziri la Lebanon kwa mara ya tatu sasa katika kipindi cha miaka minne ya hivi karibuni. Tofauti ya mara hii na mara mbili zilizotangulia yaani mwaka 2016 na 2018, ni kwamba mara hii Hariri amepata kura chache (65 tu) zinazohitajika kwa ajili ya kupewa nafasi ya kuwa Waziri Mkuu na kuunda baraza la mawaziri. Suala hili linaonyesha kuwa, tathmini ya Saad Hariri kuhusiana na suala la kuunda baraza jipya la mawaziri haikuwa sahihi. Hii ni kwa sababu kiongozi huyo na waungaji mkono wake wamefanya jitihada kubwa za kutaka kuonesha kwamba Saada Hariri ndiye mtu pekee anayeweza kuunda serikali mpya ya Lebanon. Kupewa kura 65 tu za imani ya wawakilishi wa Bunge la Lebanon kumeonyesha kuwa Hariri atakuwa na kibarua kigumu katika jitihada zake za kuunda serikali mpya. 

Saad Hariri

Kuhusiana na suala hilo jarida la Foreign Policy limeandika kuwa: "Je, matatizo ya Lebanon na hali ya nchi hiyo si ndivyo vilivyomfanya Saad Hariri ajiuzulu? Ni kwa nini basi amerejea tena kwenye cheo hicho?" Kwa hakika sababu za kuongezeka upinzani dhidi ya Hariri ni kwamba alipokuwa waziri mkuu katika miaka ya nyuma, Lebanon ilisumbuliwa na matatizo, na alilazimika kujizulu kutokana na maandamano na malalamiko mengi ya wananchi. Matatizo hayo ya Lebanon bado yako palepale, bali hata yameshadidi na kuongezeka.

Sababu nyingine ya kuakhirishwa zoezi la kuundwa baraza la mawaziri la Hariri kama tulivyosema, ni mapendekezo yake kuhusu muundo wa baraza lenyewe. Hariri anasisitiza suala la kuundwa baraza la mawaziri la mateknokrati na wataalamu wasiokuwa na mirengo ya kisiasa bila ya kujali mchango na nafasi ya vyama vya siasa. Pendekezo hilo lilibuniwa na Ufaransa na lilijadiliwa na kupasishwa baada ya mlipuko wa bandari ya Beirut wakati wa safari ya Rais Emmanuel Macron nchini Lebanon.

Hariri na Macron

Pendekezo hilo limekabiliwa na upinzani mkubwa, kwa sababu Saad Hariri mwenyewe si mteknokrati bali ni mwanasiasa. Zaidi ni kwamba, baadhi ya mirengo ya kisaisa ya Lebanon kama ule wa Free Patriotic Movement unaoongozwa na Gebran Bassil, inataka kuundwe baraza mseto la mawaziri linalojumuisha wanasiasa na mateknokrati. Sambamba na hayo Marekani, Ufaransa na Saudi Arabia zinanyemelea fursa ya kuingilia kati mchakato na zoezi la uundwaji wa serikali mpya ya Lebanon. Nchi hizo zina nia ya kutumia baraza la mawaziri la mateknokrati kama wenzo wa kuitenga harakati ya Hizbullah katika siku za usoni na kuiondoa kabisa katika muundo wa utawala wa Lebanon.

Macron

Pendekezo jingine lililotolewa na Saad Hariri kwa ajili ya muundo wa baraza la mawaziri la serikali ya Lebanon ni kundwa baraza litakalokuwa likibadilishana zamu za uongozi baina ya makundi mbalimbali ya Lebanon. Televisheni ya Al Jadeed imeripoti kuwa: "Saad Hariri amewasilisha mpango wa kugawa nafasi za wizara za serikali baina ya makundi tofauti (ya kikabila au kidini) ya Lebanon". Ripoti hiyo imesema kuwa kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baina ya Hariri na Rais Michel Aoun wa Lebanon, nafasi zote za wizara za serikali zitakuwa zikigawanywa kwa zamu baina ya makundi mbalimbali ya Lebanon isipokuwa Wizara ya Fedha ambayo inadhibitiwa na makundi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Kusimamia wizara za serikali ya Lebanon kwa zamu baina ya makundi mbalimbali ni jambo jipya ambalo halijawahi kufanyika nchini humo. Vilevile fikra hiyo ya kugawa na kusimamia wizara za serikali kwa misingi ya ukabila, udini na kadhalika litazidisha migawanyiko ya kikabila, kidini na kikaumu na kuchochea zaidi hitilafu za kisiasa nchini humo.