Skyline International Foundation: Saudi Arabia iwaachia huru wafungwa wa kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64470
Shirika la kimataifa la Skyline International Foundation lenye makao yake makuu Stockholm nchini Sweden limeitaka jamii ya kimataifa kuishinikiza serikali ya Saudi Arabia ili iwaachie huru makumi ya wafungwa wa kisiasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 07, 2020 02:30 UTC
  • Skyline International Foundation: Saudi Arabia iwaachia huru wafungwa wa kisiasa

Shirika la kimataifa la Skyline International Foundation lenye makao yake makuu Stockholm nchini Sweden limeitaka jamii ya kimataifa kuishinikiza serikali ya Saudi Arabia ili iwaachie huru makumi ya wafungwa wa kisiasa.

Shirika hilo la kimataifa limesisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa na jumuiya nyingine za kimataida zinapaswa kuchukua hatua za maana za kusitisha ukiukaji mkubwa wa uhuru na haki za binadamu nchini Saudia na kuanzisha uchunguzi kuhusu kesi za kutiwa nguvuni raia kwa kosa na kutumia uhuru wao wa kijieleza na kusema.

Skyline International Foundation imesema kuwa, Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuweka vizuizi vikubwa vya mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii kwa kuzuia kabisa mitandao hiyo au kuwahukumu kifungo au kuwatoza faini watumiaji wake kwa lengo la kuziba sauti za wapinzani. 

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo limesema kuwa, utawala wa Saudi Arabia unawatia nguvuni watu kwa kutegemea sheria ya makosa ya mtandao ambayo mashirika mengi ya kutetea haki za binadamu yanasema inawatia hatiani watu wanaoikosoa serikali katika mitandao ya kijamii. 

Baadhi ya wanaharakati wa masuala ya kijamii wa kike wanaoshikiliwa jela Saudi Arabia

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa mwenendo huo wa serikali ya kifalme ya Riyadh unapingana na sheria za kimataifa zinazohusiana na haki za kiraia na kisiasa. 

Saudi Arabia inakabiliwa na ukosoaji mkubwa wa jamii ya kimataifa kutokana na rekodi yake mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu, na inashikia jela idadi kubwa ya wasomi, wanazuoni wa kidini, wanaharakati wa masuala ya kijamii na waandishi wa habari.