Faili la mlipuko wa Beirut na hitilafu za kisiasa nchini Lebanon
Hivi karibuni kulitangazwa habari ya faili linalohusiana na mlipuko wa Agosti 4 mwaka huu katika bandari ya Beirut nchini Lebanon.
Itakumbukwa kuwa, Jumanne jioni ya tarehe 4 Agosti milipuko miwili ilitokea katika bandari ya Beirut kwenye maghala yaliyokuwa yamehifadhi shehena ya tani 2,500 za mada za amoniamu naitreti. Milipuko hiyo ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 200 na wengine zaidi ya 6,000 kujeruhiwa.
Mlipuko huo ulikuwa moja ya matukio makubwa ya kiusalama nchini Lebanon baada ya lile la 2005 la kuuawa Rafiq al-Hariri aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo wakati huo. Baada ya kuuawa Rafiq al-Hariri, kuliundwa mahakama ya kimataifa kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo na waliohusika na jinai hiyo ambapo siku chache tu baada ya tukio hilo, mahakama husika ilitangaza uamuzi wake.
Licha ya kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ilisafishwa na faili hilo, lakini mahakama hiyo kabla ya kila kitu iliathiriwa mno na matashi ya kisiasa ambapo wapinzani wa ndani na nje wa harakati hiyo waliituhumu Hizbullah mara chungu nzima kwamba, ilihusika na jinai hiyo na hivyo kufanya kila wawezalo kuipaka matope harakati hiyo ya muqawama.
Inaonekana kuwa, faili la mlipuko wa bandari ya Beirut nalo linaelekea kukubwa na hatima kama ya mahakama ya Rafiq al-Hariri, kwani katika siku za hivi karibuni, makundi na shakhsia wa kisiasa nchini Lebanon wamelazimika kujitetea kutokana na tuhuma wanazoandamwa nazo.
Fadi Sawan, Jaji wa faili la mlipuko wa bandari ya Beirut juma lililopita aliwatuhumu baadhi ya viongozi wa sasa na wa zamani kwamba, walihusika katika mlipuko huo wa Agosti mwaka huu. Fadi Sawan sambamba na kutoa agizo la mashtaka aliwatuhumu Hassan Diab, Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito, Ali Hassan Khalil, Waziri wa zamani wa Fedha, Ghazi Zaiter, Waziri wa Usafiri na Uchukuzi na Yusuph Finyanus Waziri wa Ajira za Umma kwamba, walifanya uzembe na kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na hivyo kusababisha kuaga dunia na kujeruhiwa mamia ya watu.
Kabla ya hapo pia, maafisa wa usalama, wa bandari na ushuru wa forodha wa Lebanon wapatao 30 walitiwa mbaroni wakihusishwa na mlipuko huo wa Agosti 4 mwaka huu. Agizo hilo la mashtaka la Jaji Fadi Sawan limekabiliwa na radiamali mbalimbali ndani ya Lebanon.
Baadhi ya vyombo vya habari na mirengo ya kisiasa inadai kwamba, Rais Michel Aoun wa nchi hiyo ameingilia mwenendo wa faili hilo, ingawa haijafahamika hasa uingiliaji huo umefanyika kwa madhara au manufaa ya nani. Pamoja na hayo, ofisi ya Rais Michel Aoun imetangaza katika taarifa yake kwamba: Rais Aoun hajaingilia kwa karibu wala kwa mbali mchakato wa uchunguzi unaofanywa na Jaji wa faili la mlipuko wa bandari ya Beirut, bali alichokitaka ni kuharakishwa mwenendo wa uchunguzi huo na kutangazwa haraka waliohusika na tukio hilo.
Inaonekana kuwa, tuhuma dhidi ya Rais Michel Aoun kwamba, ameingilia mchakato wa faili hilo zina uhusiano na kukataa kwake orodha ya Baraza la Mawaziri iliyowasilishwa na Waziri Mkuu Saad al-Hariri. Mwezi Oktoba mwaka huu Saad al-Hariri alipewa jukumu la kuunda Baraza la Mawaziri na kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, juma lililopita aliwasilisha majina ya serikali mpya kwa Rais Michel Aoun ambayo yamekatiwa.
Jambo jingine ni radiamali ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon. Baada ya Jaji Fadi Sawan kuwatuhumu Hassan Diab na mawaziri wengine wa serikali yake, Hizbullah ilitoa taarifa na kutangaza kwamba, hatua zozote zinazochukuliwa na Jaji anayechunguza faili la mlipuko wa bandari ya Beirut zinapaswa kuwa mbali kabisa na matashi ya kisiasa na malengo maalumu na badala yake ziwe zinaendana kikamilifu na sheria pamoja na katiba ya nchi. Kwa maneno mengine ni kuwa, Hizbullah ilitaka kusema kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba, uchunguzi wa faili hilo umegubikwa na matashi ya kisiasa.
Kwa kuzingatia ushahidi huu inaonekna kuwa, katika mwenendo wa kushughulikia faili la mlipuko wa bandari ya Beirut kama ilivyokuwa katika kadhia ya Mahakama ya Rafiq al-Hariri, uadilifu umekuwa muhanga wa maslahi ya kisiasa ya baadhi ya wanasiasa na mirengo ya kisiasa ya Lebanon na wakati huo huo, baadhi ya madola ajinabi nayo yamekuwa na ushawishi katika faili hili.