Kutoka malalamiko hadi mpasuko ndani ya chama; Netanyahu katika mashinikizo makubwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65214-kutoka_malalamiko_hadi_mpasuko_ndani_ya_chama_netanyahu_katika_mashinikizo_makubwa
Maandamano ya wiki ya 25 mtawalia dhidi ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Utawala haramu wa Israel yamefanyika juma hili katika hali ambayo, chama cha Likud kinachoongozwa na mwanasiasa huyo kimekumbwa na mgawanyiko mkubwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 15, 2020 23:26 UTC
  • Kutoka malalamiko hadi mpasuko ndani ya chama; Netanyahu katika mashinikizo makubwa

Maandamano ya wiki ya 25 mtawalia dhidi ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Utawala haramu wa Israel yamefanyika juma hili katika hali ambayo, chama cha Likud kinachoongozwa na mwanasiasa huyo kimekumbwa na mgawanyiko mkubwa.

Hivi sasa Netanyahu anakabiliwa na hali mbaya ya kisiasa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel). Yamepita majuma 25 ya maandamano dhidi ya Netanyahu. Waaandamanaji walalamikia hali mbaya ya uchumi ambayo imeshadidi zaidi baada ya kuenea virusi vya Corona.

Waandamanaji hao wanaamini kuwa, kashfa za ufisadi zinazomkabili Netanyahu kwa upande mmoja na hatua yake ya kung’ang’ania madaraka kwa upande wa pili ni mambo ambayo yameifanya serikali yake kutoyapa umuhimu matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wakazi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kwa muktadha huo, raia wa Kizayuni kwa majuma 25 mtawalia wameandamana wakisitiza kwamba, Netanyahu anapaswa kujiuzulu na kujiweka kando na siasa. Kile ambacho kimeyafanya maandamano haya kuwa na umuhimu na kushika kasi takwa la kujiuzulu Netanyahu ni kwamba, maandamano haya yamekuwa yakifanyika licha ya mlipuko wa virusi vya Corona katika ardhi hizo za Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu).

Maandamano dhidi ya Benjamin Netanyahu ambapo waandamanaji wanamtaja kuwa ni Waziri wa Jinai

 

Matatizo mengine yanayomkabili Netanyahu yanahusiana na kuongezeka mizozo na hitilafu ndani ya Baraza la Mawaziri. Kuanzia Aprili 2020 ambapo Netanyahu na Benny Gantz walifikia makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, anga ya kutoamianiana ilikuwa imeligubika baraza hilo la mawaziri tangu awali. Hiyo ilitokana na kuwa, Benny Gantz kiongozi wa chama cha Blu na Nyeupe alikuwa na shaka kama Netanyahu atakabidhi cheo cha Waziri Mkuu kwa mshirika wake huyo baada ya miezi 18 kama walivyoafikiana.

Hitilafu hizo zilishika kasi zaidi baada ya kuibuka mzozo kuhusiana na bajeti, kwani Netanyahu alikuwa akisisitiza kuandaliwa bajeti ya mwaka mmoja huku Gantz akitaka bajeti ya miaka miwili.

Gantz ambaye ni Waziri wa Vita wa Israel anaamini kuwa, Netanyahu kwa kupasisha bajeti ya mwaka mmoja anataka kulivunja Baraza la Mawaziri la utawala huo ghasibu kabla ya kumalizika muda wake wa miezi 18 na kuitisha uchaguzi wa mapema wa Bunge.

Benny Gantz, wziri wa Vita wa Israel na hasimu wa kisiasa wa Netanyahu

 

Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Gantz ameamua kumtangulia Netanyahu na kupendekeza kuvunjwa Bunge la Israel, pendekezo ambalo limepasishwa katika hatua ya awali na hivyo kuandaa uwanja wa uwezekano wa kufanyika uchaguzi wan ne wa Bunge ambao utakuwa wa mapema kuliko wakati mwingine wowote ule katika kipindi cha miezi minane ya hivi karibuni.

Jambo hilo limepelekea kushtadi mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Benjamin Netanyahu kiasi kwamba, amelazimika kuakhirisha safari yake ya kuelekea Imarati kutokana na kuweko uwezekano wa kuvunjwa Bunge la Israel, safari ambayo ilikuwa na umuhimu kwa Netanyahu kwa ajili ya maonyesho yake ya kisiasa.

Kundi la tatu la matatizo yanayomkabili Netanyahu ni changamoto ndani ya chama chake cha Likud ambazo zimeongeza mno katika siku za hivi karibuni. Kabla ya hapo yaani Desemba mwaka uliopita wa 2019, kulifanyika uchaguzi ndani ya chama cha Likud kufuatia ukosoaji ulioibuka dhidi ya chama hicho. Hivi sasa mtindo wa kuibuka hitilafu umebadilika ambapo Gideon Saar na waitifaki wake wamejitenga na chama cha Likud.

Gideon Saar mpinzani mpya wa Benjamin Netanyahu aliyetangaza kukihama chama cha Likud

 

Kabla ya kukihama chama hicho Saar alisema kuwa, kuondoka katika chama hicho maana yake ni ‘kupiga kura ya kutokuwa na imani’ na Baraza la Mawaziri la Netanyahu na kwamba, kama chama cha Likud kitapata wingi wa kura katika uchaguzi ujao wa Bunge basi atajiunga na upinzani na kwamba, hatomuunga mkono Netanyahu katika juhudi zake za kuwania tena nafasi ya Waziri Mkuu.

Kwa kuzingatia hali hii, inaonekana kuwa uchaguzi wa kabla ya wakati wa Bunge ni jambo ambalo haliendani kabisa na maslahi binafsi ya Netanyahu, kwani hata kama chama chake cha Lukud kitapata ushindi katika uchaguzi huo, bado Netanyahu atalazimika kuchuana na wagombea watatu muhimu kwa ajili ya kuwania Uwaziri Mkuu yaani Avigdor Lieberman, Benny Gantz na Gideon Saar. Hivyo tunaweza kusema kuwa, waitifaki wa jana wa Netanyahu ambao ni washindani wake wa leo wameazimia kwa dhati kabisa kumng’oa mwanasiasa huyo katika wadhifa wa Uwaziri Mkuu.