Nukta muhimu katika hotuba ya Sayyid Hassan Nasrallah
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65697-nukta_muhimu_katika_hotuba_ya_sayyid_hassan_nasrallah
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah alihutubu Ijumaa usiku kwa njia ya moja kwa moja katika televisheni ambapo hotuba hiyo ilikuwa na nukta nne muhimu za kitaifa na kimataifa.
(last modified 2026-05-19T09:45:50+00:00 )
Jan 10, 2021 21:09 UTC
  • Nukta muhimu katika hotuba ya Sayyid Hassan Nasrallah

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah alihutubu Ijumaa usiku kwa njia ya moja kwa moja katika televisheni ambapo hotuba hiyo ilikuwa na nukta nne muhimu za kitaifa na kimataifa.

Katika hotuba yake hiyo Sayyid Hassan Nasrallah aliashiria tukio la hivi karibuni ya kuhujumiwa jumba la Bunge la Congress nchini Marekani. Sawa na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Sayyid Hassan Nasrallah anaamini kuwa, yaliyojiri Jumatano iliyopita katika Congress ya Marekani ni sawa na yale ambayo Marekani imekuwa ikipanga kutekeleza dhidi ya nchi zingine zikiwemo Iran na Lebanon lakini mara hii rais wa Marekani ametekeleza  njama ndani ya nchi hiyo. Tofauti hapa ni kuwa, Marekani imekuwa ikifanya hivyo kwa kuingilia mambo ya ndani ya nchi zingine ili kuziangusha serikali zilizopo madarakani lakini katika yaliyojiri Congress hakukuwa na uingiliaji wowote wa nchi ya kigeni.

Kuhusiana na nukta hii, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: "Kilichojiri katika Congress ya Marekani ni tukio muhimu; tukio sawa na hilo lilikuwa limepangwa dhidi ya Lebanon kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Kile kilichojiri katika Congress ni sawa na kile ambacho watawala wa Marekani walikuwa wamezoea kukifanya katika nchi zingine ili kuangusha serikali za nchi hizo."

Wanamgambo wa Trump wakiwa ndani ya Bunge la Congress

Nukta nyingine ambayo Sayyid Hassan Nasrallah ameashiria kuhusu tukio la Congress ya Marekani ni kuhusu shakhsia ya Donald Trump. Kwa shakhsia na hulka yake isiyo ya kidiplomasia, ya ubinafsi na ya kuvunja sheria, Trump amezisababishia hasara kubwa nchi zingine kwa muda wa miaka minne lakini hadi sasa Wamarekani wengi walikuwa hawajafahamu utambulisho halisi wa Trump. 

Kiongozi wa Hizbullah amekosoa vikali vitendo vya Marekani katika miaka ya hivi karibuni ikiwa ni pamoja na mauaji ya makamanda wa harakati za muqawama na mapambano ya Kiislamu hasa mashahidi Qassem Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis. Ameongeza kuwa: "Yale ambayo Wamarekani na walimwengu wameshuhudia katika siku za hivi karibuni ni mfano mdogo tu wa jinai za Trump duniani katika miaka minne iliyopita huko Syria, Iraq, Yemen na jinai ya kuwaua makamanda wa muqawama Haj Qassem na Abu Mahdi al Muhandis."

Kuhusiana na masuala ya ndani ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrallah aliashiria nukta tatu ambazo ni mlipuko wa bandari ya Beirut, kuendelea vita vya vyombo vya habari dhidi ya Hizbullah na kuundwa baraza jipya la mawaziri.

Kuhusiana na mlipuko uliojiri katika Bandari ya Beirut mwezi Agosti mwaka jana, Sayyid Hassan Nasrallah amesema tukio hilo lilitumiwa kueneza propaganda zisizo na ukweli kuwa eneo hilo lilikuwa na maghala ya makombora ya Hizbullah. Amekosoa kutomalizika uchunguzi kuhusu tukio hilo baada ya miezi sita na kuongeza kuwa familia za waliouawa bado hazijajua ni vipi mada ya ammonium nitrate iliyosababisha mlipuko huo ilikuwa imewekwa katika bandari hiyo. Amesema makamanda wa Jeshi la Lebanon na wakuu wa idara zinginezo za usalama wanapaswa kuwajibika katika tukio hilo na waweke wazi ripoti za uchunguzi.

Mlipuko katika Bandari ya Beirut

Maudhui nyhingine ambayo Sayyid Hassan Nasrallah aligusia ni vita vya vyombo vya habari dhidi ya Hizbullah kupitia kuenezwa taarifa bandia. Hivi karibuni meli moja ilinaswa Italia ikiwa na dawa za kulevya. Vyombo kadhaa vya habari vilidai kuwa mihadarati hiyo ilikuwa milki ya Hizbullah. Katibu Mkuu wa Hizbullah  amesema asili ya habari ni kuwa mihadarati hiyo ni ya kundi la kigaidi la ISIS lakini vyombo vya habari  vya maadui vikageuza ukweli na kudai ni ya Hizbullah.

Nukta ya mwisho ambayo Sayyid Hassan Nasrallah aliashiria ni kutoundwa baraza la mawaziri nchini Lebanon. Baadhi nchini Lebanon wamekuwa wakidai kuwa Hizbullah imekuwa ikipoteza wakati katika kadhia hiyo ili utawala wa Trump umalizike  na hivyo mashinikizo ya kuunda baraza la mawaziri pasina kuwepo Hizbullah yapungue.  Amesema tathmini hiyo si sahihi kwani katika miaka ya hivi karibuni uundwjai baraza la mawaziri Lebanon umekuwa ukichukua muda mrefu. Kile ambacho kimezuia kuundwa baraza la mawaziri Lebanon ni mrengo wa Machi 14 ambao unapuuza uhalilisia wa mambo kisiasa kwa kujaribu kuhodhi madaraka. Kwa hivyo madai yaliyotolewa dhidi ya Hizbullah hayana msingi.