Syria yalalamika kuhusu jinai zinazofanywa na magaidi wanaopata himaya ya Marekani
Syria imesema wanaotenda jinai dhidi ya watoto wa Syria wakiwemo magaidi na wanamgambo wa Kikurdi wa SDF wanapata himaya ya Marekani.
Bashar al-Jaafari Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ambaye pia ni mwakilishi wa kudumu wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa ametoa kauli hiyo leo Jumamosi alipohutubu katika kikao kisicho rasmi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambacho kimefanyika kwa njia ya video. Kikao hicho kimeitishwa kujadili maudhi ya 'Watoto katika mapigano ya silaha'. Al-Jaafari amesema magaidi na wanagambo wa SDF ambao wanapata himaya ya jeshi vamizi la Marekani wametenda jinai dhidi ya watoto wa Syria ikiwa ni pamoja na kuwaua, kuwateka nyara na kuwapeleka katika maeneo ya kivita. Aidha amesema magaidi na wanamgambo hao wanaopata himaya ya Marekani wameteketeza moto au kuharibu shule na mahospitali.
Al-Jaafari amesema pamoja na kuwepo mashinikizo mengi, serikali ya Syria inajitahidi kuwalinda na kuwapa himaya watoto katika maeneo ambayo yamekombolewa kutoka makucha ya magaidi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria pia ameashiria matatizo wanayokumbana nayo watoto wa Syria kufuatia jinai za kigaidi na wavamizi wa kigeni hasa Marekani na waitifaki wake wa Ulaya na kusema hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na kuwa nchi nyingi ambazo raia wao ni magaidi wa kundi la ISIS waliokamatwa Syria zimekataa kuwapokea tena raia hao wakiwemo watoto.
Wanamgambo wa Kikurdi wa SDF wanaopata himaya ya kifedha na kijeshi kutoka Marekani wameteka maeneo kadhaa ya kaskazini mwa Syria na wanatenda jinai dhidi ya watu wa maeneo hayo.