Hamas, Arab League zakaribisha uamuzi wa ICC dhidi ya Israel
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepongeza hukumu ya hivi karibuni ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye maslahi kwa wananchi wa Palestina na iliyoughadhabisha mno utawala wa Kizayuni wa Israel.
Taarifa ya Hamas imesema kuwa, hukumu hiyo ya ICC ni hatua moja mbele kuelekea katika mchakato wa kuhakikisha kuwa wahanga wa ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina unaofanywa na Wazayuni wanapata haki na usawa. Katika hukumu hiyo ya juzi Ijumaa, majaji wa ICC walisema kuwa, mahakama hiyo ina haki ya kisheria ya kufuatilia jinai na uhalifu uliofanywa na Wazayuni katika ardhi za Palestina mwaka 1967.
Wakati huo huo, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imepokea kwa mikono miwili hukumu hiyo ya ICC ya kusema kuwa ina mamlaka ya kisheria ya kuchunguza jinai za Wazayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Naibu Katibu Mkuu wa Arab League anayeshughulikia masuala ya Palestina na ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu, Saeed Abu Ali amesema hukumu hiyo ni ushindi mkubwa kwa jitihada za taifa la Palestina za kuzishinikiza taasisi za kisheria na kidiplomasia za kimataifa, kuhakikisha kuwa Wapalestina wanapata haki zao za msingi.
Amesema anatumai uamuzi huo wa ICC utatoa mchango mkubwa kwa jitihada za kuasisiwa taifa huru la Palestina na kuhitimishwa uporaji na ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina unaofanywa na Wazayuni maghasibu.
ICC ilisema katika hukumu hiyo ya Ijumaa kuwa, ardhi za Wapalestina zilizoghusubiwa na Wazayuni mwaka 1967 zinajumuisha eneo lote la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ikiwemo Baytul Muqaddas Mashariki, Ukanda wa Gaza n.k, na kwamba vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni vilivyojengwa, vinavyojengwa na vitakavyojengwa kwenye ardhi hizo ni haramu na ni kinyume cha sheria.