Jeshi la Afghanistan laua wanachama 153 wa Taliban
Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imetangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limewaua wanachama zaidi ya 150 wa kundi la Taliban katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Katika ujumbe wa Twitter wa leo Jumamosi, wizara hiyo imesema mbali na wanachama 153 wa Taliban kuuawa, wengine 23 wamejeruhiwa katika operesheni kadhaa za Jeshi la Taifa la Afghanistan (ANA).
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imeongeza kuwa, operesheni hizo zimefanyika katika mikoa ya Kandahar, Ningarhar, Balkh, Zabul, Wardak, Khost, Konduz na Helmand na kwamba wamefanikiwa kutegua mabomu 38 ya kuelekezwa kutoka mbali ya kundi hilo.
Machafuko yametanda katika miezi ya karibuni kila pembe ya Afghanistan hususan mjini Kabul huku mazungumzo ya amani yanayofanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha kati ya Taliban na serikali ya Kabul yakikosa natija.
Katika miezi ya karibuni, shakhsia kadhaa mashuhuri na muhimu nchini Afghanistan wakiwemo wanasiasa, wanaharakati, waandishi wa habari, madaktari na waendesha mashtaka wameuawa mchana kweupe mjini Kabul na katika miji mingine ya nchi hiyo.
Maafisa wa serikali wamekuwa wakilituhumu kundi la Taliban kuhusika na mauaji hayo, lakini kundi hilo linakanusha tuhuma hizo. Baadhi ya mauaji hayo yamekuwa yakihusishwa pia na kundi la kigaidi la ISIS.