Lebanon katika mzingo wa hitilafu; mkwamo wa kuunda Serikali unaendelea
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66918-lebanon_katika_mzingo_wa_hitilafu_mkwamo_wa_kuunda_serikali_unaendelea
Licha ya kupita miezi minne tangu Saad Hariri kupewa jukumu la kuunda serikali nchini Lebanon, lakini Waziri Mkuu huyo hadi hivi sasa ameshindwa kuunda Baraza la Mawaziri kutokana na hitilafu na mivutano mingi iliyomo nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2021 05:29 UTC
  • Lebanon katika mzingo wa hitilafu; mkwamo wa kuunda Serikali unaendelea

Licha ya kupita miezi minne tangu Saad Hariri kupewa jukumu la kuunda serikali nchini Lebanon, lakini Waziri Mkuu huyo hadi hivi sasa ameshindwa kuunda Baraza la Mawaziri kutokana na hitilafu na mivutano mingi iliyomo nchini humo.

Tarehe 14 Februari 2021, kwa mara nyingine Saad Hariri alilalamikia kile alichokiita ni ukwamishaji wa baadhi ya watu na makundi katika juhudi zake za kuunda Serikali. Kwa upande wake ofisi ya upashaji habari ya Rais Michel Aoun wa Lebanon imetoa taarifa na kumlaumu vikali Saad Hariri ikisema kuwa, hotuba yake imejaa makosa, migongano na madai yasiyo sahihi. Taarifa ya ofisi hiyo ya Rais wa Lebanon imesema, Saad Hariri amekusudia kufanya bidaa na kulibebesha taifa la Lebanon mila na desturi ngeni zinazopingwa na misingi na katiba na ambazo zinavuruga hati ya mshikamano wa kitaifa ya Lebanon.

Kwa mara nyingine Lebanon iliingia kwenye mgogoro wa kisiasa tangu mwezi Oktoba 2019. Wakati huo Saad Hariri alilazimika kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuuu kutokana na maandamano na malalamiko makubwa ya wananchi. Hata baada ya Rais Michel Aoun kumpa tena Saad Hariri jukumu la kuunda serikali, lakini Waziri Mkuu huyo wa Lebanon ameonesha wazi kuwa nia yake ni ya kuyashinikiza makundi mengine likiwemo la Miche Aoun yakubaliane na matakwa yake hivyo amekwama kuunda Serikali. Kabla ya kupewa tena jukumu la kuunda Serikali, cheo cha Waziri Mkuu alipewa Hassan Diab, hata hivyo Saad Hariri na makundi yake yalikwamisha kikamilifu juhudi za Diab za kuunda Serikali. Mripuko mkubwa uliotokea tarehe 4 Agosti 2020 uliofuatiwa na maandamano ya wananchi, ulimlazimisha Hassan Diab kujiuzulu.

Saad Hariri anashutumiwa kwa kupokea amri kutoka nje hasa Saudi Arabia

 

Baada ya hapo aliteuliwa Mustafa Adib kuwa Waziri Mkuu wa Lebanon, lakini na yeye pia aliamua kujiuzulu mwezi mmoja tu tangu kuteuliwa kwake na hivyo kwa mara nyingine, Saad Hariri akapewa jukukmu la kuunda Baraza la Mawaziri akiwa Waziri Mkuu mpya. Hata hivyo, hadi hivi sasa Hariri ameshafanya vikao 14 na Rais Michel Aoun lakini wameshindwa kufikia mapatano ya kuundwa Serikali.

Amma swali muhimu linalojitokeza hapa ni, kwa nini licha ya kufanyika vikao vyote hivyo 14 lakini imeshindikana kuundwa baraza jipya la mawaziri huko Lebanon? Tatizo la kuundwa serikali mpya nchini humo, liko wapi?

Inavyoonekana ni kwamba tatizo kuu ni kukosekana kuaminiana baina ya Michel Aoun na Saad Hariri. Gazeti la al Bannaa la nchini Lebanon limeandika: Tatizo la kushindwa kuundwa Serikali nchini Lebanon halitokani na tofauti kuhusu nani apewe nafasi gani na nani achukue wizara gani, tatizo ni kukosekana kikamilifu imani baina ya Hariri kwa upande mmoja na Aoun na Gebran Bassil kwa upande wa pili.

Amma ni nini chanzo cha kukosekana kuaminiana baina ya pande hizo mbili? Chanzo chake ni kwamba Saad Hariri anataka kuhodhi masuala ya kisiasa na kuwatia nguvu wafuasi wake. Hariri anaonesha wazi kwamba lengo lake ni kuwavunja nguvu wafuasi wa kambi ya muqawama licha ya kwamba kambi hiyo ndiyo inayoipa kinga ya kutovamiwa Lebanon na Wazayuni na mabeberu wengine. Kama si kambi hiyo ya muqawama, leo hii Saad Hariri asingelikuwa na uthubutu huo wa kutaka kuvunja nguvu kundi na watu fulani na kuwatia nguvu watu wake.

Rais Michel Aoun wa Lebanon

 

Tatizo jengine kubwa ni kwamba Saad Hariri hayuko huru katika maamuzi yake. Ni tegemezi wa madola ajinabi na watu baki ambao hawalitakii kheri taifa la Lebanon. Misimamo ambayo imekuwa ikichukuliwa na Saad Hariri inaonesha wazi kuwa misimamo yake anapangiwa madola ya kigeni. Mfano wa wazi ni tukio la mwezi Nobemba 2017 ambapo baada ya kushinikiwa na Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Saad Hariri alijiuzulu ghafla nafasi yake ya Waziri Mkuu, ili kuisambaratisha na kuitimbukiza kwenye mgogoro mkubwa Lebanon.

Jengine ni kwamba Saad Hariri anataka kuunda serikali ambayo itawashirikisha watu wa makundi na pande zote. Rais Michel Aoun anasema, hatua hiyo ni kinyume na katiba na inakinzana na hati ya mshikamano wa kitaifa ambayo inasema, lazima Waziri Mkuu wa Lebanon atoke kati ya Waislamu wa Kisuni wa nchi hiyo, Rais atoke kwa Wakriston na Spika wa Bunge atoke kwa Waislamu wa Kishia. 

Tunapozingatia yote hayo tutaona kuwa, mgogoro wa kuundwa serikali mpya nchini Lebanon hauna dalili za kumalizika hivi karibuni. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Sayyid Ibrahim Amin al Sayyid, Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Hizbullah ya Lebanon akasema kuwa, ni jambo lililo mbali kuweza kuundwa Baraza la Mawaziri na serikali mpya nchini Lebanon hivi sasa.