Mfadhili mkuu wa kifedha wa Daesh atiwa mbaroni mkoani Diyala, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i67064-mfadhili_mkuu_wa_kifedha_wa_daesh_atiwa_mbaroni_mkoani_diyala_iraq
Idara ya Intelijinsia ya Jeshi la Iraq imetangaza habari ya kutiwa mbaroni mfadhili mkuu wa kifedha wa kundi la Daesh mkoani Diyala mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 20, 2021 08:05 UTC
  • Mfadhili mkuu wa kifedha wa Daesh atiwa mbaroni mkoani Diyala, Iraq

Idara ya Intelijinsia ya Jeshi la Iraq imetangaza habari ya kutiwa mbaroni mfadhili mkuu wa kifedha wa kundi la Daesh mkoani Diyala mashariki mwa nchi hiyo.

Idara ya Intelijinsia ya jeshi la Iraq jana Ijumaa ilitangaza kuwa, wamefanikiwa kumtia mbaroni katika eneo la  al Tabaj katika kijiji cha Khanaqin mtu aliyekuwa akiwafadhili pakubwa kifedha magaidi wa Daesh.

Mfadhili huyo mkuu wa Daesh amekamatwa kupitia oparesheni ya kiintelijinsia ya aina yake na kwa mujibu wa taarifa za siri walizopewa na kupitia uratibu uliofanyika kati ya idara ya intelijinsia ya kamandi ya oparesheni ya mkoa wa Diyala na vitengo vinginevyo vya upepelezi jeshini. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gaidi huyo ambaye alikuwa akisakwa kwa mujibu wa kipengee cha nne cha sheria ya kupambana na ugaidi, ametiwa nguvuni akiwa na fedha aina ya dinari na dola.  

Kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq cha Hashdu Shaabi katika mwaka mmoja wa karibuni kimekuwa na nafasi kuu na athirifu katika kukabiliana na mashambulizi ya masalia ya magaidi wa Daesh katika mikoa mbalimbali ya Iraq; na khususan katika mkoa wa Diyala mashariki mwa nchi hiyo.

Wapiganaji wa Hashdu Shaabi 

Masalia hayo ya Daesh yamezidisha hujuma na mashambulizi yao katika siku za karibuni dhidi ya wapiganaji wa Hashdu Shaabi huko Diyala. Magaidi wa Daesh wanaendelea kuungwa mkono na Marekani ili kuendelea kutekeleza hujuma zao katika maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Diyala.