Saudia yazidi kushutumiwa kwa kuvunja haki za binadamu
Dada wa mwanaharakati mmoja wa masuala ya kijamii wa Saudi Arabia ameushutumu vikali utawala wa ukoo wa Aal Saud kwa kuwatesa na kuwakandamiza wakosoaji wa utawala huo wa kiimla.
Lina Alhathloul, dada wa Loujain Alhathloul, mmoja wa wanaharakati wa masuala ya kijamii wa Saudi Arabia ameiambia televisheni ya CNN ya Marekani kwamba ukoo wa Aal Saud unaendelea kuvunja haki za binadamu, kuwakandamiza na kuwatesa vibaya wakosoaji wa utawala huo wa kidikteta na kuongeza kuwa, dada yake yaani Loujain Alhathloul alipewa mateso makali yaliyosimamia na Saad al Qahtani, mmoja wa watu wa karibu wa Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia.
Lina Alhathloul aidha amesema katika mahojiano hayo kwamba hali ya haki za binadamu katika nchi ya Saudi Arabia inayodhibitiwa na Mohammed bin Salman, ni mbaya sana.
Loujain Alhathloul (31) alikuwa anashikiliwa katika jela za ukoo wa Aal Saud tangu mwezi Mei 2018 na tarehe 26 Oktoba alipigwa marufuku kuwasiliana na watu wa familia yake. Kosa pekee alilofanya mwanamke huyo wa Saudia kwa mtazamo watawala wa nchi hiyo, ni kutaka kwake wanawake waruhusiwe kuendesha gari nchini Saudi Arabia. Mwendesha Mashataka mkuu wa Saudia amemshtaka mwanaharakati huo kwa kile alichodai ni kuhatarisha manufaa ya taifa.
Utawala wa kidikteta wa Saudi Arabia una historia ndefu mbaya ya kuwatia mbaroni, kuwateka nyara, kuwaua na kuwatesa wakosoaji wa serikali na wanaharakati wa masuala hata ya kijamii.