Mji mkuu wa Saudia, Riyadh washambuliwa kwa kombora,milipuko yasikika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i67346-mji_mkuu_wa_saudia_riyadh_washambuliwa_kwa_kombora_milipuko_yasikika
Muungano wa kivita wa Saudia, unaotekeleza hujuma dhidi ya Yemen, umedai kuwa umetungua kombora kabla halijatua katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh. Baadhi ya duru zimesema milipuko kadhaa imesikika katika mji huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 28, 2021 01:12 UTC
  • Mji mkuu wa Saudia, Riyadh washambuliwa kwa kombora,milipuko yasikika

Muungano wa kivita wa Saudia, unaotekeleza hujuma dhidi ya Yemen, umedai kuwa umetungua kombora kabla halijatua katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh. Baadhi ya duru zimesema milipuko kadhaa imesikika katika mji huo.

Kanali ya Televisheni ya Saudia ya Al Arabia Jumamosi usiku imenukulu taarifa ya muungano huo ikisema kituo cha cha ulinzi wa anga kimezima shambulizi la kombora dhidi ya Riyadh.

Msemaji wa muungano wa kivita wa Saudia, Turki Al Maliki amedai kuwa Harakati ya Ansarullah ya Yemen imevurumisha kombora la balistiki kuelekea Riyadh na kwamba kombora hilo limetunguliwa kabla halijatua lilikolengwa.

Saudia imedai kutungua kombora hilo katika hali ambayo, vyombo vya habari vimewanukulu mashuhuda wakisema milipuko kadhaa imesikika mjini Riyadh.

Hadi sasa Jeshi la Yemen halijatoa taarifa yoyote kuhusiana na shambulio hilo.

Hivi karibuni, maafisa wa serikali ya Yemen wamesema nchi yao hivi sasa imo vitani, inashambuliwa kila uchao na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia, hivyo ni haki ya kawaida kabisa kwa wananchi wa Yemen kujibu mashambulizi wanayofanyiwa.

Mji wa Riyadh

Wiki iliyopita, Muhammad Ali Al-Houthi, mwanachama mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen alisema Jeshi la Yemen,  likishirikiana na Kamati za Wananchi, litaendelea kutumia makombora na ndege zisizo na rubani kutekeleza hujuma ndani kabisa ya ardhi ya Saudia na waitifaki wake. 

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwaka 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen wakiongozwa na Harakati ya Ansarullah.

Harakati hiyo, kwa kushirikiana na Jeshi la Yemen, imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya ardhi ya Saudi Arabia ambapo imelenga mara kadhaa vituo vya kusafisha mafuta na pia viwanja vya ndege vinavyotumiwa na jeshi vamizi la utawala huo wa kifalme.