Bin Salman na jinamizi la Khashoggi
Serikali ya Marekani imechapisha baadhi ya nyaraka za siri zinazohusiana na mauaji ya kinyama ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa Saudi Arabia aliyekuwa akiishi Marekani na kutangaza kuwa jinai hiyo ilitekelezwa kwa amri ya moja kwa moja ya Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia.
Ni kwa msingi huo ndipo viongozi wa Marekani wakasema kuwa hawatazungumza tena moja kwa moja na mwanamfalme huyo. Kufuatia tangazo hilo, swali hili linaulizwa kwamba je, uamuzi huo wa serikali ya Marekani utakuwa na taathira gani kwa mustakbali wa kisiasa wa Bin Salman?
Maudhui ya kwanza ni kuwa suala hilo bila shaka litaadhoofisha nafasi ya kisiasa ya mwanamfalme huyo ndani ya Saudia. Mrithi huyo wa kiti cha ufalme ambaye alikuwa na matumaini makubwa kutoka kwa serikali iliyoondoka madarakani ya Donald Trump alipata pigo kubwa kwa kumpoteza muungaji mkono wake huyo mkubwa baada ya kushindwa rais huyo mwenye utata mwingi katika uchaguzi mkuu wa Marekani. Kuchapishwa ripoti ya mauaji ya Khashoggi kwa mara nyingine tena kumeanika wazi utambulisho wa kikatili wa Bin Salman. Kwa msingi huo, fikra iliyopo hivi sasa katika ukoo wa Aal Saud ni kwamba kukalia mwanamfalme huyo kiti cha ufalme kutaharibu sura ya nchi hiyo katika ngazi za kimataifa. Hivyo suala hilo linatazamiwa kuongeza harakati za kupinga utawala wake wa baadaye nchini humo.
Maudhui ya pili ni kwamba kuna uwezekano wa Bin Salman kuwekewa vikwazo vya kimataifa. Kwa msingi huo ripota wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mauaji ya Khashoggi amesema kwamba kufukuzwa wale wote waliotoa amri ya kuuawa Khashoggi katika uwanja wa kimataifa ni hatua muhimu katika utekelezaji uadilifu, na kuwa hatua hiyo bila shaka itatoa ujumbe mzito kwa viongozi wengine ambao wana mawazo ya kutekeleza jinai kama hiyo. Ripota huyo ameongeza kwamba: Tunaiomba White House isisimamishe tu mali za Bin Salman bali iiwekee vikwazo miamala yake yote ya kimataiafa.
Hata kama ni jambo lililo mbali kwa sasa kwa serikali ya Marekani kumuwekea vikwazo Bin Salman lakini ni wazi kuwa mashinikizo ya fikra za waliowengi duniani dhidi ya mwanamfalme huyo yataongezeka katika siku zijazo.
Maudhui ya tatu ni kwamba tishio la kupoteza fursa ya kuketi kwenye kiti cha ufalme wa Saudia mbayo ni ndoto ya muda mrefu ya Bin Salman, litaimarisha zaidi nafasi ya washindani wake katika ukoo wa Aal Saud. Serikali ya sasa ya Marekani ina mtazamo na upendeleo maalumu kwa Muhammad bin Nayef, mrithi wa kiti cha ufalme wa zamani wa Saudia, ambaye nafasi yake imedhoofishwa sana na Bin Salman. Kuhusu hilo Bruce Riedel mhadhiri katika chuo cha Brookings anaandika kwamba: Jamii ya kimataifa sasa inapasa kudai kuachiliwa huru Muhammd bin Nayef, mrithi wa zamani wa kiti cha ufalme wa Saudia. Hakufungwa kutokana na kuwa alifanya kosa, bali ni kwa kuwa alikuwa akimsababishai matatizo Muhammad bin Salman, mrithi wa sasa wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo.
Muhammad bin Naif aliokoa makumi, kama si malefu ya roho za Wamarekani na kuishinda al-Qaida nchini kwake. Huenda mashinikizo yanayotolewa sasa na Washington dhidi ya watawala wa Saudia, likaonekana kuwa si jambo la kawaida lakini ni wazi kuwa kushughulikiwa kwa haraka jambo hilo ni muhimu kwa kitilia maani kuwa utajiri mkubwa wa Naif katika kudhamini usalama wa Wamarekani ni maudhui inayozingatiwa sana na viongozi wa Washington.
Nukta ya mwisho ni kwamba, tukiachilia mbali taathira za ripoti ya mauaji ya kinyama ya Khashoggi kwa mustkabali wa kisiasa wa Bin Salman, na kwamba ndiye aliyetoa amri ya moja kwa moja ya kuuawa mwandishi habari huyo mpinzani wa utawala wa Aaal Saud, ni wazi kuwa hatua hiyo inathibitisha kwa mara nyingine kuwa mwanamfalme huyo hajaiva kisasa. Hivyo, ni wazi kuwa anapasa kuanza kufanya tena juhudi za kuiridhisha Marekani ili aimarishe nafasi yake ya kuwa mfalme wa baadaye wa Saudi Arabia. Mara hii huenda utajiri mkubwa wa dola za mafuta alizonazo usiweze kumuokoa.