Jeshi la Yemen latungua ndege ya kijasusi ya Saudi Arabia
Jeshi la Yemen limetangaza kutungua ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya Saudi Arabia wakati ikiwa katika oparesheni ya kijasusi nchini humo.
Vyombo vya habari vya Yemen vimeripoti kuwa ndege hiyo isiyo na rubani ya muungano wa kivita unaoongozwa na Saudia imetunguliwa katika eneo la Al Hadida.
Haya yanajiri wakati ambao hivi karibuni muungano vamizi wa Saudia ulitekeleza shambulizi dhidi ya nyumba ya makazi katika eneo la al-Hok mkoani Al Hudayda ambapo raia watano wa familia moja waliuawa.
Hivi karibuni mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Answarullah ya Yemen amesisitiza kuwa, harakati hiyo itaendelea kuishambulia miji na maeneo ya Saudi Arabia maadamu ukoo wa Aal Saud unaendelea kuishambulia miji ya Yemen.
Muhammad al Bukheiti ameongeza kuwa, operesheni za makombora dhidi ya Saudia zitaendelea hadi pale dola hilo vamizi litakapoacha mashambulizi na kuizingira Yemen kila upande. Amesema, hiyo itakuwa hatua ya kwanza na ni baada ya hapo ndipo San'aa itakuwa tayari kufanya mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro huo ulioanzishwa na Saudi Arabia.
Ikumbukwe kuwa kuanzia Machi 2015, Saudi Arabia kwa uungaji mkono wa Marekani, Umoja wa Falme za Kiarbau na nchi kadhaa zingine ilianzisha hujuma ya kijeshi dhidi ya Yemen na kuizingira nchi hiyo angani, nchi kavu na baharini.
Ndege za kivita za Saudia na watifaki wake hadi sasa zinaendeleza mashambulizi dhidi ya Yemen ambapo makumi ya maelfu ya raia, hasa wanawake na watoto wameuawa na mamilioni ya Wayemen wamelazimika kuwa wakimbizi.