Al Houthi: Saudia itaangamia ikiendelea kuishambulia Yemen
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mapinduzi Yemen amesisitiza kuwa iwapo Saudi Arabia itaendeleza hujuma yake dhidi ya Yemen, uvamizi huo utapelekea kuangamia ufalme wa Saudia.
Kwa mujibu wa Televisheni ya Al Mayadeen, Muhammad Ali al-Houthi amesisitiza kuwa kudumishwa amani ya kweli kutategemea kusitishwa mzingiro na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen.
Wakati huo huo, Msemaji wa Majeshi ya Yemen Brigedia Jenerali Yahya al-Sari alisema Jumatatu kuwa jeshi hilo limefanikiwa kulenga kwa makombora maeneo kadhaa ya Saudia ikiwa ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Abha katika wilaya ya Asri.
Juzi vikosi vya ulinzi vya Yemen vilifanikiwa kuyalenga maeneo iliyoyakusudia katika mipaka ya mashariki ya Saudi Arabia katika oparesheni ya ulipizaji kisasi.
Katika oparesheni hiyo ya Jumapili, ndege 14 zisizo na rubani (droni) na makombora 8 ya balistiki ziliipiga taasisi ya mafuta ya Saudia ya Aramco katika bandari ya mafuta ya Ras al Tanura na maeneo mengine ya kijeshi huko Dammam.
Aidha , kambi kadhaa za kijeshi za Saudia katika maeneo ya Aseer na Jizan nazo pia zilishambuliwa na droni nne kwa makombora saba aina ya Badr.
Msemaji wa Majeshi ya Yemen alibainisha kuwa, mashambulio hayo ni utumiaji wa haki ya wazi na kisheria ya wananchi wa Yemen ya kujibu ushadidishaji wa hujuma na mashambulio pamoja na mzingiro wa kila upande iliowekewa nchi yao na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.