Mar 10, 2021 02:19 UTC
  • Nukta kadhaa kuhusu safari ya Papa Francis huko Iraq

Safari ya siku tatu ya Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani huko Iraq ambayo ilianza Ijumaa iliyopita imemalizika.

Kuna umuhimu hapa wa kutaja nukta kadhaa kufuatia kumalizika safari hiyo tajwa. Nukta ya kwanza ni kuwa; Papa Francis hana mamlaka ya utekelezaji kuhusiana na maamuzi yanayohitajia dhamana ya utekelezaji. Kwa msingi huo, tangu awali haikutarajiwa kuwa safari  ya Papa huko Iraq ingezaa matunda ya kiutekezaji, bali safari hiyo imekuwa na taathira za kihistoria na kimaonyesho tu. Ndio maana kiongozi huyo wa Wakristo wa Kikatoliki duniani akafanya safari katika nchi ya Kiislamu yenye jamii kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Kishia na kukutana na kufanya mazungumzo na Marja Taqlidi wa Waislamu hao. Kwa msingi huo, hata kama masuala kama vile ya kuzikurubisha pamoja dini mbalimbali, kuzuia machafuko, ubaguzi wa kidini na kupambana na ugaidi yamesisitizwa kwenye safari hiyo ya Papa Francis huko Iraq, lakini matamshi hayo zaidi ya yote yameweka wazi daghadagha walizonazo viongozi wa dini huku utekelezaji na utatuzi wa masuala hayo ukitegemea irada ya kisiasa ya serikali ya Iraq; na taaba'an hali ya ndani ya nchi hiyo.  

Nukta nyingine ni kuwa, wapo baadhi wanaoamini kuwa safari ya Papa huko Iraq imepelekea kupata nguvu nafasi ya Hauza ya Najaf katika Ulimwengu wa Kishia. Mtazamo huu unabainishwa kwa lengo kuu la kuibua kambi na mirengo miongoni mwa maraji mbalimbali katika ulimwengu wa Kishia. Hii ni kwa sababu Hauza ya Najaf na Ayatullah Sistani mwenyewe wana hadhi na daraja ya juu; na safari ya Papa haiathiri kivyovyote vile nafasi hiyo. Nafasi hiyo adhimu ndiyo iliyompelekea Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani kuamua kufunga safari hadi nyumbani kwa Ayatullah Sistani ili kufanya naye mazungumzo. Fikra hiyo eti ya kupanda daraja nafasi ya Hauza ya Najaf inatajwa lengo kuu likiwa ni kuzusha hitilafu kati ya hauza nyingine za kielimu katika Ulimwengu wa Kishia; jambo ambalo hata hivyo limesambaratishwa kwa kutolewa taarifa na Jumuiya ya Walimu na Watafiti wa Hauza ya Kielimu ya mji mtukufu wa Qum.  

Papa Francis akiwa nyumbani kwa Ayatullah Sistani huko Iraq 

Nukta ya tatu kuhusu safari hiyo, ni mtazamo wa kisiasa. Anga ya kisiasa ya Iraq khususan hivi sasa imegubikwa na mivutano na malumbano kati ya makundi mbalimbali; na serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mustafa al Kadhimi pia iko chini ya mashinikizo makubwa. Hata kama suala la kudhaminiwa usalama katika safari hiyo ya kihishoria ni rekodi chanya ya utendaji wa serikali ya al Kadhimi, hata hivyo haionekani kuwa safari hiyo imekuwa na mchango maalumu wa kisiasa kwa serikali ya Baghdad na Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Bali kilichopo ni jitihada zinazofanywa na waungaji mkono wa serikali ili kunufaika kisiasa na safari hiyo.  

Wakati huo huo serikali ya kieneo ya Arbil huko Kurdistan pia inafanya jitihada za kisiasa ili kwa mara nyingine tena kudhihirisha wazi miongoni mwa fikra za waliowengi msimamo wa Wakurdi na serikali hiyo ya kieneo ya Kurdistan. Muhammad Amin Panjuini mwanasiasa Mkurdi wa Iraq anasema kuhusu ziara ya Papa huko Arbil kwamba: Safari ya Papa huko Arbil imeakisiwa pakubwa kimataifa; na yeye amekuwa mgeni wa Wakurdi katika safari hiyo, na  hiyo inaaminisha kuwa kadhia ya Wakurdi, haki na matakwa yao yote kwa mara nyingine tena yamewekwa wazi katika duru za kimataifa. Hii ni katika hali ambayo sababu kuu iliyompelekea Papa Francis kufanya safari huko Arbil ni kutokana na kuwepo idadi kubwa ya Wakristo katika eneo la Kurdistan. Kwa hiyo Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani amelitembelea eneo la Kurdistan kwa ajili ya kufuatilia masuala ya Wakristo na pia kukutana na kufanya mazungumzo na Waksristo wa eneo hilo. 

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani akutana na Wakristo wa Arbil 

Nukta ya mwisho ni kuwa; hata kama safari ya Papa huko Iraq imekuwa ni ya utambulisho wa kidini lakini imeonyesha namna dini zote zinavyoheshimu amani, usalama, na heshima ya mwanadamu na kupinga pakubwa machafuko; na iwapo kuna matatizo makuu katika upande wa utekelezaji; hilo linahusiana na udhaifu na kukosekana irada thabiti za serikali ndani ya nchi na kwa mataifa makuu duniani.

Tags