Ansarullah: Makombora yetu ni jinamizi kwa wavamizi wa Yemen
Mjumbe mmoja wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, makombora ya balestiki ya nchi hiyo ni jinamizi kwa maadui.
Ali al Qahoom amesema hayo usiku wa kuamika leo wakati alipohojiwa na televisheni ya al Mayadeen na kuongeza kuwa, ndoto za Saudia za kulishinda taifa la Yemen zimeshindwa kuaguka na kwamba taifa la Yemen hivi sasa lina nguvu zisizotabirika za kijeshi. Amesema, nguvu za vikosi vya ulinzi vya Yemen pamoja na uwezo wa kijeshi wa harakati ya Ansarullah unaongezeka siku baada ya siku.
Mjumbe huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah pia amesema, taifa la Yemen lina machaguo mengi katika medani ya mapambano akisisitiza kuwa, Saudi Arabia kamwe haiwezi kulishinda taifa la Yemen kwani lina machaguo na nguvu nyingi zisizotabirika.

Siku za hivi karibuni, vikosi vya ulinzi vya Yemen vimeshambulia kambi kadhaa za kijeshi na vituo mbalimbali vya mafuta ndani kabisa ya ardhi ya Saudi Arabia. Shambulio la karibuni kabisa ni dhidi ya uwanja wa ndege wa Abha na bandari kubwa ya kusafirisha mafuta ya Saudi Arabia ya Ras Tanura.
Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia kwa msaada wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, nchi za Ulaya na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen na kuwazingira kila upande wananchi hao wasio na hatia. Saudia ilianzisha uvamizi na mashambulizi hayo ya kikatili kwa ndoto na tamaa ya kuidhibiti Yemen katika kipindi cha wiki chache tu. Hata hivyo huu ni mwaka wa 6 na kila kukicha wananchi wa Yemen wanazidi kupiga maeneo muhimu na nyeti ndani kabisa ya Saudia.