Mripuko wa bomu waua watu wasiopungua 64 mjini Baghdad, Iraq
Watu wasiopungua 64 wameuawa na wengine zaidi ya 85 wamejeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea leo karibu na soko moja katika kitongoji cha Sadr mashariki mwa mji mkuu wa Iraq, Baghadad.
Kwa mujibu wa duru za Iraq bomu hilo lilikuwa limetegwa kwenye gari lililokuwa limeegeshwa karibu na soko la Urayda.
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limetangaza kuwa ndilo lililohusika na shambulio hilo.
Inafaa kuashiria kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita vikosi vya jeshi la Iraq vimepata mafanikio makubwa katika kuwaangamiza na kuwatimua magaidi wa kundi la Daesh katika maeneo mengi ya ardhi ya nchi hiyo yaliyokuwa yamevamiwa na kushikiliwa na magaidi hao na kufanikiwa kuikomboa miji muhimu kadhaa ikiwemo Baiji, Tikrit na al-Ramadi.
Hivi sasa jeshi la Iraq limeanzisha operesheni ya kuukomboa mji wa Faluja katika mkoa wa al-Anbar ukifuatiwa na Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa kaskazini mwa nchi hiyo.
Katika upande mwengine vikosi vya jeshi la Iraq leo asubuhi vimefanya operesheni kubwa ya mashambulio kwa lengo la kulikomboa eneo la al-Baghdadi magharibi mwa mkoa wa al-Anbar ulioko magharibi mwa nchi hiyo.../