Russia yasisitiza udharura wa Syria kurejeshewa uanachama wake katika Arab League
(last modified Tue, 13 Apr 2021 02:51:35 GMT )
Apr 13, 2021 02:51 UTC
  • Russia yasisitiza udharura wa Syria kurejeshewa uanachama wake katika Arab League

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesisitiza udharura wa Syria kurejeshewa uanachama wake katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Lavrov ametoa sisitizo hilo Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na mwenyeji wake, waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry mjini Cairo na akaeleza kwamba, Russia inatilia mkazo umuhimu wa Syria kuanza tena kuwa mwanachama wa Arab League.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amebainisha kuwa, Syria ni sehemu ya Ulimwegu wa Waarabu na akaongeza kwamba, katika mazungumzo yake na waziri mwenzake wa Misri yaliyogusa masuala mbali mbali, wamejadili pia kadhia ya Syria na haki ya watu wa nchi hiyo kujiamulia mustakabali wao.

Rais Bashar al-Assad wa Syria

Itakumbukwa kuwa mwaka 2011 na kufuatia kuanza mgogoro na vita nchini Syria, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ikishinikizwa na Saudi Arabia, ilichukua hatua ya kusimamisha uanachama wa Syria; na nchi nyingi za Kiarabu zikaamua kufunga balozi zao mjini Damascus na kukata uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo.

Baada ya serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria kupata ushindi kwa kuyasambaratisha magaidi na kuzima njama ya pamoja ya Waarabu na Wamagharibi, Arab League na nchi nyingi wanachama wa jumuiya hiyo zikiwemo za eneo hili la Asia Magharibi zimekuwa zikihaha na kufanya juu chini ili kuanzisha tena uhusiano  na Syria na kufungua tena balozi zao mjini Damascus.../  

Tags