Saudia yawavurumishia maroketi wananchi wa Yemen
Katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa wimbi la mashambulio ya kikatili dhidi ya Yemen, muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia umeyavurumishia maroketi makazi ya raia katika mikoa kadhaa ya nchi hiyo maskini jirani yake.
Kwa mujibu wa Televisheni ya al-Masira, ndege 12 za kivita za Saudia zimelenga makazi ya raia wa kawaida kwa maroketi katika miji ya Sarwah na Madaghal.
Duru za habari zinaarifu kuwa, ndege hizo za wavamizi zimevurumisha maroketi 13 dhidi ya makazi ya wananchi wasio na hatia katika miji ya Haraz, Khaab, Ash-Sha’af na Kataf katika mikoa ya Hajjah, Al-Jawf na Saada.
Wayemen kadhaa wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya anga ya Saudia hususan katika mkoa wa Saada.
Haya yanajiri masaa machache baada ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (PGCC) kutoa taarifa hasi na iliyojaa uhasama dhidi ya harakati ya Ansarullah ya Yemen na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
PGCC pasina kuashiria chochote kuhusu uuzaji wa silaha za Marekani kwa Saudia, imedai kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kufanya jitihada za kuzuia kupelekewa silaha Jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu inayozongwa na vita tokea Machi 2015.