Zaidi ya walowezi 400 wavamia Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa
Makumi ya walowezi wa Kizayuni wameuvamia tena Msikiti wa al-Aqswa huko Palestina wakisaidiwa na askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel na kuuvunjia heshima msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.
Taarifa zaidi zinasema, walowezi wa Kizayuni zaidi ya 400 mapema leo waliuvamia msikiti wa al-Aqswa na kufanya vitendo vya kulivunjia heshima eneo hilo takatifu.
Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kwamba, hujuma na uvamizi huo umefanyika kwa msaada na uungaji mkono wa wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel.
Walowezi hao wa Kizayuni wamevamia msikiti huo na kusaidiwa na wanajeshi wa Israel katika hali ambayo, Waislamu wamekuwa wakikabiliwa na mibinyo na ukwamishaji kwa ajili ya kutekeleza ibada zao za kila siku katika msikiti huo kwa kisingizio cha virusi vya Corona.

Wakati huo huo, makundi ya muqawama na mapambano ya Palestina yameonya kuhusiana na hatua hizo za walowezi wa Kizayuni za kuuvamia na kuuvunjia heshima msikiti mtakatifu wa al-Aqswa.
Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.