Ansarullah: Inasikitisha kuona Saudia ikiwazuia Waislamu kutekeleza ibada ya Hija
(last modified Tue, 20 Jul 2021 02:58:57 GMT )
Jul 20, 2021 02:58 UTC
  • Ansarullah: Inasikitisha kuona Saudia ikiwazuia Waislamu kutekeleza ibada ya Hija

Katibu Mkuu wa harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah amesema inasikitisha kuona Saudi Arabia ikiwazuia Waislamu kutoka maeneo mengine ya dunia kutekeleza ibada ya Hija kwa mwaka wa pili mfululizo.

Sayyid Abdul Malik Badruddin al Houthi amesema usiku wa kuamkia leo kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya Idul Adh'ha kwamba, kitendo cha serikali ya Saudia ni ukiukaji wa wazi wa faradhi ya Hija ambayo Mwenyezi Mungu ametaka iwe faradhi ya Kiislamu ya dunia nzima.

Amesema kuzuia Waislamu kutekeleza ibada hiyo kunapingana na mafundisho ya Qur'ani tukufu na ni jinai na uhalifu mkubwa. Ameongeza kuwa, jambo hilo linadhihirisha nafasi haribifu ya utawala wa kifalme wa kizazi cha Aal Saud dhidi ya Umma wa Kiislamu. 

Al Houthi amesema kuwa, hatua kama hizi za utawala wa Riyadh zinafanyika kwa ajili ya kuwahudumia maadui wa Umma wa Kiislamu na zinafanyika kwa usimamizi wa Marekani na Uingereza. 

Abdul Malik Badruddin al Houthi

Serikali ya Saudi Arabia mwaka huu pia, kama ilivyokuwa mwaka jana, imewazuia mahujaji kutoka maeneo mengine ya dunia kushiriki katika ibada muhimu ya Hija katika mji mtakatifu wa Makka kwa kutumia kisingizio cha maambukizi ya corona.

Riyadh imetangaza kuwa, watu wanaoishi nchini humo pekee ndio walioruhusiwa kutekeleza ibada hiyo.